Na Ripota wetu,Tunduru
BAADHI ya wazee wa Kijiji cha Amani kata ya Namasakata Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kuongeza kasi kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu ambao umekuwa tishio na kusababisha vifo vya watu wengi hususani wazee waishio vijijini.
Wakizungumza jana wakati wa kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa wakazi wa kijiji hicho, wazee hao wameomba wataalam wa Afya waendelee na kampeni ya kijiji hadi kijiji kwani itasaidia kuibua watu wengi ambao wanashindwa kwenda Hospitali ya wilaya umbali wa km 20 kwa ajili ya vipimo pamoja na tiba ya ugonjwa huo.
Hamis Rashid(65) na Ahamd Majikita(70) licha ya kuipongeza Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kuanzisha kampeni ya uchunguzi wa kifua kikuu kwa watoto na watu wazima.
Hata hivyo walidai, kuna haja ya wataalam hao kwenda katika maeneo yote hasa vijijini ambako kuna idadi kubwa ya watu wenye viashiria vya ugonjwa wa kifua kikuu lakini hawajapata vipimo wala tiba na wanaendelea kuteseka.
Ahmad Majikita alisema, tatizo linalochangia kukithiri kwa magonjwa maeneo ya vijijini ni hali duni ya kipato, kutokana na kukosa fedha za nauli, gharama za chakula na maradhi pindi wanapohitajika kwenda Hospitali ya wilaya Tunduru au katika vituo vya Afya kwa ajili ya kupata matibabu.
Alisema,kwa hiyo kama wataalam watafika kila kijiji itasaidia wazee wengi kutambua hali ya Afya zao na kupata matibabu.
Alisema, maeneo ya vijijini wazee wengi wanapoteza maisha kwa kukosa vipimo na tiba sahihi kwani licha ya kuwepo kwa zahanati lakini tatizo ni vifaa tiba kwa ajili ya vipimo, wataalam na baadhi ya dawa ambazo zinapatakana katika hospitali ya wilaya Tunduru mjini na katika vituo vikubwa vya Afya.
Kwa upande wake mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema,serikali kupitia kitengo cha kifua kikuu katika Hospitali ya wilaya imeanza kuchukua hatua kwa kutembelea vijijini kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu sambamba na kuwaanzishia dawa wale watakabainika kuwa na vimelea vya maradhi hayo.
Kwa mujibu wa Kihongole,Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau wengine kama shirika la MDH katika kutokomeza ugonjwa huo ambao unatajwa ni miongoni mwa ugonjwa hatari unaoongoza kuuwa watu wengi Ulimwenguni.
Alisema, ugonjwa wa kifua kikuu unatibika kwa mtu kupata tiba sahihi, na makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo ni pamoja na wazee,watoto walio chini ya miaka mitano na watu wanaoishi kwenye mazingira yenye mwanga hafifu na hata hewa mzito.
Kihongole alitaja kundi lingine ni watumiaji dawa za Hospitali kwa muda mrefu bila kufuata ushauri wa kitaalam na wale wenye magonjwa sugu na utapia mlo kwa watoto wadogo.
Dkt Kihongole ameshauri wananchi kwenda kufanyiwa vipimo vya afya zao mara kwa mara badala ya kukimbilia kununua dawa na kumeza au kusubiri hadi pale hali inapokuwa mbaya kwani ni hatari kwa usalama wao.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Amani kata ya Namasakata Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,wakimsikiliza mratibu wa kifua kikuu na Ukoma wa Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole(hayupo pichani)wakati wa zoezi la uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa wakazi wa kijiji hicho,hata hivyo wazee hao wameiomba Serikali kukiongezea nguvu kitengo cha kkifua kikuu na Ukoma ili wataalam wake waweze kufika maeneo mengi kwa ajili ya uchunguzi wa ugonjwa huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...