Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii.
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mwita Waitara amesema Serikali imejipanga vema kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika mwaka huu unakuwa huru na wa haki huku ikisisitiza hakuna sababu ya kuwepo kwa hofu ya aina yoyote.
Akizungumza leo Septemba 5, 2019 bungeni Mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu, Waitara ametumia nafasi hiyo kueleza namna ambavyo Serikali imejipanga kufanikisha uchaguzi huo na kuwatoa hofu Watanzania wote.
Maelezo hayo ya Waitara yalitokana na swali la msingi la Mbunge wa Kibamba jijini Dar es Salaam John Mnyika ambaye alitaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kupeleka mabadiliko ya Katiba kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.
"Mbunge Mnyika kwa nafasi yako ya ubunge unayo nafasi ya kuleta hayo mabadiliko na Bunge litayapokea na kujadili.Hata hivyo kanuni, miongozo na taratibu ziko wazi , uchaguzi wa Serikali ya Mtaa utasimamia na Waziri mwenye dhamana na si vinginevyo.
Wakati wa kuandaa kanuni za uchaguzi wa Serikali ya Mtaa wadau wakiwamo wa vyama vya siasa walikuwepo.Hata Naibu Katibu Mkuu wa Chadema naye alikuwepo na kanuni ya uchaguzi huo na muongozo wa mpiga kura amekabidhiwa.Hata hivyo katika kutoa maoni si lazima yote yachukuliwe , wataalam wanachambua na kuangalia lipi wachukue na lipi waache,"amesema Waitara.
Amefafanua hakuna sababu ya wananchi kuwa na hofu na uchaguzi na si mara ya kwanza kufanya nchini kwani kwa muda mrefu nchi yetu imekuwa ikifanya uchaguzi huo tena kwa uhuru na haki.
Akizungumza zaidi kuhusu hofu, amesema ni kweli kuna hofu isiyo na sababu imejengekeka na hivyo kuendelea kuwaomba wananchi kuondoa hofu hiyo."Hakuna sababu ya kuwa na hofu , binafsi nimewahi kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kivule nikiwa Chadema.
"Na nimewahi kuwa mbunge nikiwa huko huko Chadema, hii inaonesha namna uchaguzi ulivyokuwa huru na haki kwani nilishinda na nikawa kwenye nafasi hizo,"amesema.
Hata hivyo amesema kuwa kupitia kanuni ya uchaguzi wa Serikali ya Mtaa imeeleza kwa kina nani anastahili kusimamia uchaguzi huo na kwa mazingira hayo ifahamike Serikali imejipanga vizuri kuusimamia uchaguzi huo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...