Charles James, Michuzi TV

JIJI la Dodoma limetajwa kuongoza katika kundi la Halmashauri za Majiji kwa kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 13.0 huku Jiji la Mbeya likiwa la mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya Shilingi Bilioni 2.7.

Takwimu hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo wakati akitoa taarifa ya mapato ya vyanzo vya ndani vya halmashauri kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka ya mwezi Julai hadi Septemba.

Waziri Jafo pia ameipongeza pia Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga kuwa imekua ya kwanza Kitaifa kwa kukusanya mapato kwa asilimia 52 huku Halmashauri ya Kyerwa ya mkoani Kagera ikishika nafasi ya mwisho kwa kukusanya kwa asilimia tatu ya makisio yake.

Katika kuzipima halmashauri zote kwa pamoja katika kipindi hiki imeonesha kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekusanya mapato mengi zaidi kuliko halmashauri zote kwa kukusanya Bilioni 13.10 na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ikishika mkia kwa kukusanya Shilingi Milioni 35.15.

" Kuna halmashauri ambazo kwa upande wa asilimia tumesema Msalala imekua ya kwanza lakini ukiangalia lile pato ghafi Jiji la Dodoma limeonekana ndio la kwanza ikifuatiwa na Manispaa ya Ilala ambayo imekusanya Bilioni 13.0.

Hawa Buhigwe wa mkoani Kigoma wamekusanya Shilingi Milioni 35 tu kwa kipindi chote hiki cha miezi mitatu, sasa taarifa za kimkoa zinaonesha Mkoa wa Rukwa umekua wa kwanza kwa kukusanya pato la ndani kwa asilimia 31, wakati Mtwara umekua wa mwisho kwa asilimia kwa kukusanya asilimia 13 ya mapato yake ya ndani," Amesema Mhe Jafo.

Kwa upande wa mapato ya ndani ya halmashauri kimkoa kwa kuzingatia wingi wa mapato, Mhe Jafo amesema Mkoa wa Dar es Salaam ndio ulioongoza kwa kukusanya Shilingi Bilioni 39.5 na Mkoa wa mwisho katika wingi wa ukusanyaji wa mapato ni Mkoa wa Kigoma ambao umekusanya Shilingi Bilioni 2.1 katika kipindi hicho.

" Kwahiyo Mkoa wa Kigoma na halmashauri zake zote miezi mitatu wamekusanya Shilingi Bilioni mbili wakati kule Jiji la Dodoma nimezungumza wamekumapatoShilingi Bilioni 13 hawa Kigoma mkoa mzima. Kwahiyo kwa pato ghafi hawa Kigoma wameonekana ni wachovu kuliko wote hivyo niwatake wajitathimini ili waweze kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato," Amesema Jafo.

Kwa upande wa Halmashauri za Majiji kwa kigezo cha asilimia, Jiji la Dar es Salaam limeongoza kundi hili kwa kukusanya asilimia 38 ya makisio yake ya mwaka na Jiji la Dodoma limekua la mwisho katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 18 ya makisio yake.

Akizungumzia ukusanyaji wa mapato kwa Manispaa, Waziri Jafo ameitaja Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kuwa kinara kwa kukusanya asilimia 42 ya makisio yake huku Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ikishika mkia kwa kukusanya asilimia Tisa ya makisio yake kwa mwaka wa fedha 2019/20.

" Nimpongeze sana Mkurugenzi wa Sumbawanga ndugu yangu Jacob kwa kazi kubwa anayofanya toka ateuliwe, toka tumtoe Nzega amefanya maboresha makubwa Sumbawanga na leo tunaona wanafanya vizuri kwenye mapato. Kwa Kigoma Ujiji nirudie tena wanapaswa kubadilika wamekua wamwisho kwenye mapato kila kona hii ni aibu kwao," Amesema Waziri Jafo.

Ametumia nafasi hiyo kuwaonya wakurugenzi ambao hawatumii ipasavyo nafasi zao kusimamia ukusanyaji wa mapato na kueleza kuwa wanapaswa kuangalia mabadiliko yaliyofanywa na Rais Magufuli katika nafasi za Ukurugenzi kama sehemu ya wao kujitathimini kwenye nafasi wanazohudumu.

" Wale ambao wanashindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato tunawaweka katika taa nyekundu tunapigia mstari kwa kuwa wako kwenye taa nyekundu hata wenzao walikuwa kwenye taa nyekundu na walishaondoka tukaleta watu wapya, kumbukeni juzijuzi Mhe Rais alifanya mabadiliko ya baadhi ya wakurugenzi hivyo kwa wale ambao wanasuasua kwenye utendaji wao wajitathimini," Amesema Jafo.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo (katikati) akizungumza na wandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya vyanzo vya ndani vya Halmashauri kwa kipindi cha robo mwaka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...