Na Karama Kenyunko. Globu ya jamii.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alikataa kuandika maelezo polisi kuhusu watu anaodai waliuliwa na Jeshi la Polisi huko kwenye operesheni mkoani Kigoma.

Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Morogoro, SP Albert Kitundu (49) ameeleza hayo leo Oktoba 22, mwaka huu, alipokuwa akitoa ushahidi wake katika kesi ya uchochezi inayomkabili Zitto, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas simba.

Amedai katika upelelezi uliofanywa wakati huo yeye akiwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Kinondoni, alibaini kuwa kilichosemwa na Zitto hakikuwa na ukweli kwani watu waliofariki si 100 kama ilivyodaiwa bali ni wanne ikiwemo askari polisi wawili.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, shahidi huyo amedai Zitto alikamatwa na maofisa wa jeshi hilo baada ya kutoa maneno ya uchochezi na kufikishwa kituo cha Polisi Oysterbay na  kumuhoji kawaida ambapo alipoulizwa nafasi yake katika chama cha ACT Wazalendo, historia ya maisha yake na elimu aliyaeleza kwa kirefu.

Aliendelea kudai kuwa, alipomuuliza kuhusu tuhuma alizozitoa kwa jeshi hilo, alikiri kufanya mkutano na waandishi wa habari na kutoa ufafanuzi kuhusu watu 100 aliodai wameuliwa.

"Baada ya kueleza hayo nilimwambia Zitto nataka kumuhoji kama mtuhumiwa ili maelezo yake yaweze kutumika kama kielelezo mahakamani. Nilimpa haki zake lakini alisema hayuko tayari kutoa maelezo yake polisi na kudai atayatoa mahakamani," alidai SP Kitundu.

Hats hivyo shahidi Katundu alidai uwa walimuomba taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari na kuwapatia.

Shahidi huyo alidai aliongoza upelelezi wa tukio hilo kwa kupitia hotuba ya Zitto ambayo mmoja wa maofisa wa polisi aliichukua kwenye mkutano wake ambayo walikuta maneno ya kichochezi yaliyokuwa yanatakiwa kutolewa ufafanuzi na mshitakiwa huyo.

Amedai maneno yaliyotakiwa kutolewa ufafanuzi ni kwamba "jeshi la polisi limeuwa wananchi wapatao 100 na waliokwenda kutibiwa katika Zahanati ya Nguruka, polisi walichukua majeruhi na kuwaua."

Pia alidai aliwasiliana na RCO wa Kigoma na kutaka awapatie taarifa kuhusu tuhuma zilizotolewa na Zitto ambaye aliwapa maelezo ya watu mbalimbali aliowahoji ndipo akagundua kilichosemwa hakikuwa na ukweli kwani watu wanne ndio waliopoteza maisha kati yao wawili ni askari polisi na wawili ni wananchi. 

Ameendele kudai kuwa, hakuna majeruhi aliyechukuliwa na polisi na kuuawa isipokuwa waliwachukua ili kuwahoji kuhusu operesheni iliyotokea.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 22, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

Katika kesi hiyo, Zitto anadaiwa Oktoba 28, 2018 Zitto akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT Wazalendo alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Inadaiwa alisema " Watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua".

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...