Na Karama Kenyunko,  globu ya jamii

WAKUU wa vituo vya Polisi  Oysterbay na  Kijitonyama wameitikia wito na kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kueleza kwa nini mshtakiwa Elizabeth Balali (54) anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi hakupelekwa gerezani kama amri ya mahakama ilivyotaka badala yake wakakaa nae kituoni.

Wakuu hao ASP Kazwenge wa Osterbay na ASP Rujuo wa Kijitonyama walifika mahakamani hapo leo Oktoba 25,2019 kama mahakama ilivyowaagiza jana na majira ya saa tano na nusu iliingia katika chumba cha Hakimu  Mwandamizi Mfawidhi, Kevin Mhina ambapo walikaa  kwa dakika kadhaa wakiwa pamoja na Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon kisha wakatoka nje ndipo mahakama ikamuita mshtakiwa.

Mshtakiwa Elizabeth Balali alifikishwa mahakamani hapo ambapo Wakili Wankyo aliieleza mahakama kuwa upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika hivyo akaomba tarehe  nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia hatua yà upelelezi.

Kufuatia taarifa hiyo, Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 7, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na akasisitiza kuwa mshtakiwa apelekwe rumande."Kesi itatajwa tena tarehe 11, mwaka huu mshtakiwa apelekwe rumande, nasisitiza mshtakiwa apelekwe rumande" amesema Hakimu Mhina.

Jana jioni, Mahakama iliamuru wakuu hao wa vituo kufika mahakamani hapo kueleza  kwanini wamekaa na mshitakiwa kituo cha polisi badala ya kumpeleka gerezani.Oktoba 10, mwaka huu mahakama ilitoa amri kwa mshitakiwa ambaye ni msimamizi wa mirathi wa mke wa marehemu, Daudi Balali, Elizabeth Balali (54) kwenda gereza la Segerea kwa sababu anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ambayo haina dhamana.

Hata hivyo, kesi hiyo ambayo ilipaswa kuendelea jana haikuweza kusikilizwa kutokana na mkanganyiko uliokuwepo baada ya mshitakiwa huyo kubainika hakuwepo gereza la Segerea na kwamba alikuwa kituo cha polisi.

Mshitakiwa huyo aliletwa mahakamani akitokea Kituo cha Polisi Kijitonyama alikokuwa amekaa kwa siku saba na Kituo cha Oysterbay alikaa siku saba.Katika kesi hiyo, Elizabeth ambaye ni Mkazi wa Boko Magengeni,  anakabiliwa na mashtaka ya kujipatia Sh milioni 25 kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha.

Awali wakili Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai  kati ya Oktoba 19 na Desemba 21, 2017 Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia kiasi cha Sh milioni 25 kutoka kwa Dk Roderick Kisenge kwa ulaghai.Mshitakiwa anadaiwa  kujifanya anamuuzia eneo la mita za mraba 900 ambalo halijapimwa lililopo eneo la Boko Dovya Kinondoni wakati akijua eneo hilo si lake.

Wankyo alidai katika kipindi hicho  mshitakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Dk Kisenge kupitia akaunti yake iliyopo Katika Benki ya CRDB wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya kusomewa mashtaka, Elizabeth hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza makosa ya Uhujumu Uchumi na Hakimu Mhina alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa sababu mashitaka ya utakatishaji fedha hayana dhamana kisheria.

Hivyo alielekeza mshitakiwa huyo kurudishwa rumande katika gereza la segerea hadi leo kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...