Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Klabu ya Soka ya Simba imeendeleza ubabe mbele ya Azam FC baada ya kuichapa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (VPL) uliopigwa kwenye dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliokuwa wa vuta nikuvute dakika zote 90, ubabe ukitawala ndani ya dimba, Simba SC walipata matokeo hayo ya ushindi kupitia kwa Mshambuliaji wake, Meddie Kagere (MK 14) dakika ya 49 kipindi cha pili baada yakuunganisha kwa Kichwa pasi safi ya guu la kushoto ya Kiungo Mshambuliaji, Fransic Kahata.
Dakika za lala salama, Azam FC walionekana kuwa bora kutaka kusawazisha bao hilo baada yakuwaongeza Mshambuliaji, Shaaban Iddi 'Chulunda' na Donald Ngoma kuongeza mashambulizi, na kufanikiwa kuisumbua ngome ya ulinzi ya Simba ilikuwa chini ya Serge Wawa Pascal na Erasto Nyoni waliokuwa wanasaidiwa na Gadiel Michael na Haruna Shamte pembeni.
"Sisi tumengeneza nafasi nyingi sana ambazo hatukuweza kuzitumia, lakini wenzetu wamepata bahati, wametengeza nafasi chache wametumia moja na wamepata ushindi", amesema Nahodha wa Azam FC, Salum Aboubakar 'Sure Boy'.
"Ugumu wa mchezo ulikuwa, kwanza timu zote mbili ni nzuri, zote zinacheza, zinaweza kucheza, kikubwa sisi tulifuata maagizo ya Kocha wetu ndio maana tukapata ushindi huu", amesema Nahodha wa Simba FC, Erasto Nyoni.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana zilikutana August 17, 2019 kwenye mchezo wa Ngao ya Hisani, ambapo Simba SC iliibuka na ushindi wa bao 4-2 mbele ya Azam.
Kwa ushindi huo, Simba SC wanakuwa kileleni mwa msimamo wa VPL kwa alama 15 baada ya ushindi wa michezo yake mitano ya Ligi hiyo wakati Azam FC wanabaki na alama zake 9 akiwa na michezo minne.

Kikosi cha Simba FC
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...