Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (mbele) akiangalia moja ya kokoto zinazozalishwa na kampuni ya Kiswila Minerals iliyopo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro kwenye ziara yake aliyoifanya katika kampuni hiyo yenye lengo la kukagua shughuli za uzalishaji wa madini ujenzi tarehe 31 Oktoba, 2019.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (katikati mwenye kofia) akiwa katika picha ya pamoja na vikundi vya Kiwakoki na Kiwako vinavyojihusisha na shughuli za uchimbaji wa mawe kwa ajili ya kutengeneza kokoto katika eneo la Lugono Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, katika ziara yake aliyoifanya tarehe 31 Oktoba, 2019.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiswila Minerals, Ivan Kingu (kushoto) akimwongoza Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula ( wa pili kushoto) pamoja na msafara wake kwenye machimbo yake ya kokoto yaliyopo katika eneo la Mlandizi Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro tarehe 31 Oktoba, 2019.
*********************************
Na Greyson Mwase, Morogoro
Wachimbaji wa Madini Ujenzi katika Wilaya ya Mvomero wamempongeza Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula pamoja na Uongozi wa Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro kwa kuwatembelea na kutatua kero mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu.
Wachimbaji hao wametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti kwenye ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula aliyoifanya katika Wilaya ya Mvomero leo tarehe 31 Oktoba, 2019 yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ujenzi pamoja na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wa madini hayo.
Katika ziara yake Profesa Kikula aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Shija, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Morogoro (MOREMA), Dk. Omari Mzeru, Mwenyekiti wa Madini ya Ujenzi na Wachimbaji Wasio Rasmi, Aquilin Magalambula, Mkaguzi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Seif Msangi pamoja na Maafisa kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini.
Akizumza kwa niaba wa wamiliki wa machimbo ya mchanga yaliyopo katika eneo la Luwe Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, Ibrahim Zakaya alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro wameona mabadiliko makubwa kwa kuwa wamekuwa wakipata ushirikiano wa kutosha hivyo kuhisi sehemu ya wamiliki wa rasilimali za madini na kuchangia kwenye pato la taifa.
“Binafsi nimekuwa nikiwasiliana na hata kwenda kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Shija nakusaidiwa, jambo jingine ni ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula ambayo imezaa matunda kwa changamoto zetu kutatuliwa mara moja,” alisema Zakayo.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akizungumza mara baada ya kusikiliza kero za wamiliki wa machimbo hayo, alielekeza wamiliki wa machimbo kuhakikisha wanakuwa na mpango wa ufungaji wa machimbo ili kuepuka madhara ya mazingira yanayoweza kujitokeza mara baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa mchanga.
Aidha, Profesa Kikula alielekeza wachimbaji wa mchanga kuhakikisha wanafuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake ikiwa ni pamoja na kuzingatia masuala ya afya, mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa mchanga.
Katika hatua nyingine, Profesa Kikula aliwataka wamiliki wa machimbo hayo, kuwa na mikataba ya utoaji wa huduma kwa jamii inayotambulika kisheria ili kuepuka migongano inayoweza kujitokeza baina yao na wananchi wa vijiji vinavyozunguka machimbo.
Alisema kuwa ni vyema wamiliki wa machimbo hayo wakahakikisha wanaingia
makubaliano ya kisheria na wanavijiji wanaozunguka machimbo yao kuhusu utoaji wa huduma kwa jamii kama vile maji, barabara, ujenzi wa madarasa ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza mbeleni.
Awali akiwasilisha changamoto zilizopo katika machimbo hayo, Mkaguzi wa Madini ya Ujenzi katika Machimbo ya Luwe, Ester Choloi alieleza kuwa ni pamoja na baadhi ya wachimbaji wasiokuwa na leseni za madini kuvamia machimbo usiku na kuchukua mchanga kinyume na taratibu.
Wakati huohuo Profesa Kikula mara baada ya kusikiliza na kutatua kero za vikundi vya Kiwakoki na Kiwako vinavyojihusisha na shughuli za uchimbaji wa mawe kwa ajili ya kutengeneza kokoto katika eneo la Lugono Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, wachimbaji hao walimpongeza kwa kazi nzuri kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini.
“Kwa kweli sasa tunaona Sekta ya Madini inafanya kazi hasa baada ya kuona kero mbalimbali zikitatuliwa na Serikali kupitia Tume ya Madini,” alisema Mwenyekiti wa Kikundi cha Kiwakoki, Juma Makusi kwa niamba ya wenzake.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Kiwako, Barnabas Gidion mbali na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Tume ya Madini kwenye usimamizi wa rasilimali za madini
aliwasilisha kero za vikundi husika ikiwa ikiwa ni pamoja na matumizi ya vifaa duni na kuiomba Serikali kuwasaidia kupitia ruzuku.Alieleza kero nyingine kuwa ni pamoja na miundombinu mibovu ya barabara hali inayokwamisha usafirishaji wa kokoto hususan katika kipindi cha mvua.
Katika hatua nyingine Profesa Kikula alitembelea Mgodi wa Kuchimba Kokoto unaomilikiwa na Kampuni ya Kiswila Minerals uliopo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro ambapo mbali na kupongeza kampuni hiyo kwa kazi nzuri kwenye uchimbaji wa kokoto aliitaka kampuni kufanya kazi kwa kufuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.
Aliitaka kampuni kuwa mabalozi kwa wachimbaji wengine wa madini ya ujenzi kwenye uendeshaji wa shughuli zake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...