Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.
WAFANYAKAZI watatu wa kampuni ya simu za mkononi Tigo, na wafanyabiashara wawili, wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi sita nje baada ya kukiri na kutiwa hatiani kwa kosa la kutapeli wateja wa mtandao huo kwa njia ujumbe wa maandishi.
Wafanyakazi wa Tigo kutoka tawi la Mlimani City na Makao Makuu ya Kampuni hiyo waliohukumiwa ni Kokubelwa Karashani, Godfrey Magoye na Khalfan Milao ambao ni watoa huduma kwa wateja huku washitakiwa wengine ni Mohamed Abdallah na Moses Kilosa (mume wa Karashani) ambao walikuwa hawana kazi lakini walikuwa marafiki wa wafanyakazi hao wa Tigo.
Hukumu hiyo imesomwa leo Oktoba 16, 2019 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambae, amewatia hatiani washitakiwa hao baada ya kukiri kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Akisoma hukumu hiyi, hakimu Rwizile amesema amesikiliza hoja za pande zote na kwamba makosa waliyofanya washitakiwa si mepesi na kwa mujibu wa sheria anayepatikana na hatia katika makosa hayo anatakiwa kutumikia kifungo hivyo, lazima adhabu kali itolewe ili kupunguza makosa ya mtandao.
Amesema washitakiwa watatakiwa kutumikia kifungo cha miezi sita nje na pia simu 31 na laini zake pamoja na sare ya Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) vinataifishwa na kuwa mali ya serikali.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa alidai washitakiwa waliingia makubaliano na DPP hivyo hawatarajii wapewe adhabu kubwa.
Katika utetezi wao,washitakiwa hao waliiomba mahakama iwahurumie na kuwapa adhabu ndogo kwani hilo ni kosa lao la kwanza.
Awali Mbagwa alisoma hati mpya ya mashitaka ambapo mashitaka matano likiwemo la kutakatisha fedha liliondolewa na kusomewa mashitaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Akisoma mashitaka hayo, Mbagwa amedai Januari Mosi 2018 na Juni 20,2019 maeneo ya Dar es Salaam na Arusha walijipatia Sh 20,378,627 kutoka kwa wateja mbalimbali wa tigo kwa kutoa kwenye akaunti zao zao za Tigopesa bila idhini.
Mashtaka yaliyoondolewa ni, kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka katika akaunti za wateja ,kuingilia mifumo ya kifedha ya Tigo pesa bila kibali, kupatikana na mavazi ya JWTZ.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...