NA YEREMIAS NGERANGERA, NAMTUMBO
Urani ni metali ya asili yenye kawaida ya kutoa mionzi ambapo
imekuwepo ardhini tangu kuumbwa kwa dunia miaka bilioni tatu na
nusu(3,500,000,000) iliyopita.
Upatikanaji wa urani ikiwa ardhini inaanza na tani mbili na kuendelea
katika sehemu mbalimbali ikiwa ndani ya miamba , ndani ya maji ya
ardhini na baharini
Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na
makampuni ya kigeni zilifanya utafiti wa madini katika ardhi ya wilaya
ya Namtumbo mwaka 2006 na kugundua uwepo wa madini ya Urani katika mto
mkuju kijiji cha Likuyusekamaganga.
Ugunduzi wa madini ulileta matumaini kwa wananchi wa wilaya ya
Namtumbo licha ya kutolewa taarifa kuwa mionzi ya madini hayo ni
hatari kwa afya ya binadamu .
Mionzi ya madini hayo zikiingia kwenye mwili wa binadamu hufanya kazi
ya kuharibu mfumo wa ukuaji wa seli ,lakini wananchi Wilayani
Namtumbo wanalalamikia kuchelewa kuanza kwa uchimbaji wa madini ,
wakiamini kuanza kwa uchimbaji wa madini hayo kutawanufaisha kiuchumi.
Uchimbaji wa madini ya urani yenye mionzi na hatari kwa afya za
binadamu huchimbwa kwa njia ya shimo lililowazi au kwa njia ya
kuingia ndani ya ardhi yaliko madini .
Licha ya madhara yanayoelezwa na wataalamu kuhusu madini ya urani
wananchi Wilayani Namtumbo hususani vijana wanashauku kubwa ya kupata
ajira ya kuchimba madini ya urani waweze kujipatia kipato.
Madini ya Urani katika mto mkuju yanapatikana karibu na uso wa dunia
kiasi ambacho kitarahisisha uchimbaji wake na uchimbaji wa njia ya
shimo lililowazi ndio utakaotumika.
Katika Madini ya Urani kuna mionzi hatari ya aina tatu, Alfa,Beta na
mionzi aina ya Gamma kwa pamoja mionzi hiyo inamadhara kwa afya ya
binadamu iingiapo mwilini .
Mionzi aina ya Alfa ina madhara mara ishirini zaidi ya madhara
yanayoweza kutolewa na mionzi aina ya beta na gamma katika mwili wa
binadamu wakati wa uchenjuaji .
Mionzi huingia katika mwili wa binadamu kwa njia ya hewa au kwa njia
ya kumeza chembechembe za urani wakati wa uchenjuaji wa madini baada
ya kuchimbwa kutoka ardhini.
Hamu ya wananchi wa Namtumbo hasa vijana ya kupata ajira ya kuchimba
madini ya Urani licha ya madini hayo kuwa hatari kwa afya za binadamu
zinaendelea kupotea baada ya kampuni iliyotegemewa kuanzisha kuchimba
madini Mantra Tanzania Limited kutoonesha dalili za kutaka kuchimba
madini hayo.
Wananchi katika wilaya ya Namtumbo kupitia vikao vya serikali
hawajachoka kuhoji kuhusu ajira zinazosemwa kuwa kuanza kwa uchimbaji
wa madini ya urani katika mto mkuju utasaidia vijana kupata ajira huku
wakibaki bila majibu sahihi juu ya lini madini hayo yataanza
kuchimbwa rasmi.
Afisa Mahusiano wa kampuni ya Mantra Tanzania Limited Adija Pallangyo
anadai kampuni ya Mantra haijaanza uchimbaji wa madini kutokana na
madini hayo kushuka bei katika soko la dunia kiasi ambacho kitaifanya
kampuni kupata hasara endapo wataanza kuchimba madini kulingana na
gharama za uendeshaji.
Kampuni ya mantra inakadiriwa kuwepo katika eneo la mto mkuju kwa
zaidi ya miaka 12 hali inayopelekea wananchi kuhoji viongozi wa
serikali Wilayani Namtumbo mara kwa mara uwepo wao katika eneo hilo
huku hakuna shughuli za uchimbaji zinazoendelea.
Mbunge wa jimbo la Namtumbo Edwin Amandus Ngonyani pamoja na
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Daniel Magnus Nyambo
katika ziara zao za kuzungumza na wananchi Wilayani hukutana na swali
mara kwa mara linalohusiana na lini madini ya urani katika mto mkuju
yataanza kuchimbwa? Ambapo majibu yakiendelea ya kuwataka wananchi
kuendelea kuvuta subira .
Bwana Ngonyani kupitia kikao cha kamati kuu ya chama cha mapinduzi
mkoa wa Ruvuma amewafafanulia wajumbe wa kikao kuwa ajira asilimia
99.5 za vijana zinasubiriwa kupatikana katika uchimbaji wa madini ya
urani huku makampuni ya uchimbaji wa madini hayo yakiendelea kusuasua
katika uchimbaji na wananchi wameanza kupoteza matumaini juu ya
uchimbaji wa madini hayo kutokana na kusubiri kwa muda mrefu.
Wananchi Wilayani Namtumbo matumaini yao kwa kampuni ya Mantra kuwa
ingeanza kuchimba madini hayo kutokana na mwelekeo wake wa kushiriki
kikamilifu kuwezesha shughuli za kijamii na ghafla kampuni hiyo
inaonekana kuanza kutoweka taratibu kwenye kushiriki shughuli za
kijamii na kupunguza wafanyakazi waliopo kwa kiasi kikubwa na kuleta
sintofahamu kwa wananchi kuhoji kama uchimbaji wa madini hayo
utafanyika .
Wapo wananchi Wilayani hapa wanabishana wao kwa wao wakihoji uhalali
wa kampuni hiyo kukaa zaidi ya miaka 12 bila kufanya kazi ya uchimbaji
lakini pia wanabiashana kuhusu aina ya kibali kinacho tolewa na wizara
inayohusiana na madini ni cha utafiti au cha uchimbaji na kama ni cha
utafiti ni kwa muda wote huo na kama cha uchimbaji mbona uchimbaji
haufanyiki.na kuacha wananchi katika maswali magumu wakibishana wao
kwa wao.
Eneo linalotumiwa na kampuni ya Mantra lipo katika Hifadhi ya misitu
ya Undendeule (undendeule forest reserve) ambalo lina urani nyingi
wananchi wanahoji kauli ya profesa Dos Santos Silayo katibu mkuu
wakala wa misitu Tanzania aliyoitoa katika mkoa wa katavi kuwa hakuna
uchimbaji wowote wa madini utakaofanyika katika Hifadhi bila kibali
,kampuni hiyo inawezaje kukaa katika Hifadhi bila kibali na wanahoji
ni kibali gani cha utafiti au uchimbaji kinachotolewa kwa muda wa
zaidi ya miaka 12 na uchimbaji usifanyike.
Barani afrika urani huzalishwa kwa asilimia 18 ya urani yote
duniani na hatua ya uchimbaji na uchenjuaji wa urani Afrika ulianza
mwaka 1952 Afrika kusini na mwaka 1976 nchini Namibia .
Nchi za Afrika ambazo zina kiasi kikubwa cha madini ya urani ni
Algeria,Botswana,Jamhuri ya kidemokrasia ya kati , Jamhuri ya
kidemokrasia ya Kongo ,Gabon,Guinea,Eguatorial guinea,Malawi na Mali.
Zingine ni nchi ya Mauritania ,Morocco,Namibia ,Niger ,Afrika kusini
,Tanzania ,Zambia pamoja na Zimbabwe
Nchini Tanzania madini ya urani yanapatikana Wilayani
Namtumbo,Bahi,Galapo,Minjingu,Mbulu,Simanjiro,Ziwa
Natron,Manyoni,Songea,Tunduru ,Madaba na Nachingwea
Katika wilaya ya Namtumbo madini ya urani yanapatikana katika kijiji
cha Likuyuseka katika mto mkuju yenye jumla ya tani 58,500 ambayo
inaizidi wilaya zingine kwa uwingi wa urani Nchini Tanzania.
Kitendawili cha uchimbaji wa madini ya Urani katika mto mkuju Wilayani
Namtumbo kilianza kutolewa na waziri wa viwanda na biashara wa Urusi
bwana Denis Manturov kwa kudai kuwa uchimbaji wa madini ya urani
katika Mto mkuju utaanza mapema mwaka 2018 kupitia kampuni ya
Russian”s Uranium one Inc ya nchini humo.
Katika eneo la mto mkuju kampuni ya Mantra Tanzania Limited ilionekana
ndio kampuni yenye dhamira ya dhati ya kutaka kuanza uchimbaji wa
madini hayo na kuwatumainisha wananchi katika kutegemea kupata ajira
lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea na chakushangaza zaidi
wafanyakazi wa kampuni hiyo imeanza kuwaondoa wafanyakazi wake katika
eneo hilo na kuwafanya wananchi Wilayani Namtumbo kuanza kupotelewa na
matumaini ya ajira kutokana na kuchimba madini hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...