Baadhi ya watoto wakila chakula shuleni.

Na Woinde Shizza Michuzi blog,Arusha
WAZAZI wameshauriwa kuwa na desturi ya kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao mashuleni ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwani watoto wengi wamekuwa wakifeli kutokana na utoro.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa shule ya sekondari Olmotonyi Forest iliyopo kijiji cha Emaoi kata ya Olmotonyi halmashauri ya Arusha, Anna Minja wakati akizungumza na wazazi na wanafunzi katika mahafali ya 4 ambapo jumla ya wanafunzi 141 walihitimu .

Anna amesema kuwa changamoto kubwa ambayo imekuwa ikizikabili shule nyingi ni kutokana na wazazi kutochangia fedha kwa ajili ya chakula cha mchana kwa watoto wao hali ambayo huchangia kuwepo kwa utoro kwa watoto ambao hawali mashuleni.

Amesema kuwa kutokana na baadhi ya wazazi wengi kutokuwa na mwamko wa kuchangia chakula mashuleni, kumekuwa kukichangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuwepo kwa division ziro shuleni hapo, hivyo amewaomba wazazi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa ajili ya elimu ya watoto wao kwa kuchangia fedha kwa ajili ya chakula ili watoto waweze kusoma kwa utulivu.

"Kwa kweli uwepo wa baadhi ya wazazi wengi kutochangia chakula cha mchana kwa ajili ya watoto wao ndio wamekuwa wakichangia shule yetu kupata wanafunzi wenye division ziro, kwani wengi wa wanafunzi wanaopata ziro na wale ambao hawali chakula cha mchana hapa shuleni, hivyo tunawaomba sana wazazi wachangie chakula cha watoto ili tuhakikishe tunafuta division ziro."alisema Anna.

Aidha amesema kuwa shule hiyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upungufu wa madarasa sita ,nyumba za walimu saba,maabara moja,bwalo la chakula, vyoo vya wasichana, maktaba, pamoja na walimu wa masomo ya Sayansi.

"Tunaomba serikali utusaidie ujenzi wa mabweni mawili kwa ajili ya wavulana kwani mabweni yaliyopo ni kwa ajili ya wasichana tu,kwani wavulana wanaendelea kupata adha kubwa sana ya kuwahi shuleni kutokana na kutembea umbali mrefu ."alisema Anna.

Naye Meneja msaidizi wa Hifadhi ya misitu Meru/ Usa, Jeremiah Gumadi amewataka wanafunzi hao kujitahidi kusoma kozi mbalimbali za kujiajiri ili kuweza kukabiliana na changamoto ya ajira iliyopo hivi sasa,huku akiwataka kutochagua kazi .

Aidha amewataka kujifunza zaidi maswala mbalimbali ya ujasiriamali ambayo yatawawezesha wao kuweza kujiajiri wenyewe na kujipatia kipato badala ya kutegemea kuajiriwa.

Kwa upande wa wanafunzi waliohitimu, Hawa Jaffary na Charles Mbowe wamesema kuwa, kitendo cha kuwepo kwa shule katika mazingira hayo kumeleta manufaa makubwa kwa jamii hiyo kwa kuondoa mrundikano wa wanafunzi katika shule zingine za kata.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...