Viongozi waandamizi wa muugano wa Tanzania Election Alliance (TanEA ) pichani, kulia Mwenyekiti wa Muungano huo Michael Kyande,Katibu wa Taasisi ya The Right Way (TRW),Gideon Mazara,Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Action for Change (ACHA),Bi.Martina Kabisama pamoja na Mwenyekiti wa ACHA Justina Shauri wakionesha vijarida vya elimu ya Uraia na Uchaguzi vitakavyosambazwa kwa Wananchi baada ya kuzindua Muungano wao leo Novemba 1,2019 jijini Dar es Salaam.Picha na Michuzi JR (MMG).
Viongozi waandamizi wa muugano wa Tanzania Election Alliance (TanEA ) pichani wakishuhudia Mwenyekiti wa Muungano huo Michael Kyande (kulia), akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa Muungano huo leo Novemba 1,2019 jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Action for Change (ACHA),Bi.Martina Kabisama akizungumza leo Novemba 1,2019 jijini Dar es Salaam
wakati wa uzinduzi wa Muungano wa Tanzania Election Alliance (TanEA ) wenye lengo la kutoa elimu ya Uraia na Uchaguzi kwa Wananchi kwa kuanza na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Action for Change (ACHA) Justina Shauri akifafanua jambo katika uzinduzi huo leo Novemba 1,2019 jijini Dar es Salaam

Mratibu wa muugano wa Tanzania Election Alliance (TanEA ) ,Rhoda Kamungu akiwakaribisha wageni waalikwa pamoja na mgeni rasmi wakati wa uzinduzi huo,uliofanyika leo Novemba 1,2019 jijini Dar es Salaam
Viongozi waandamizi wa Tanzania Election Alliance (TanEA ) wakifuatilia jambo wakati wa uzinduzi huo leo Novemba 1,2019 jijini Dar es Salaam
Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamii
TAASISI ya Action For Change(ACHA) na Right Way (TRW) waungana kwa pamoja na kuzindua muungano wao
unaofahamika kwa jina la Tanzania Election Alliance kwa lengo la kushirikiana
kwa pamoja kutoa elimu ya uraia na kueleza kuwa katika kutekeleza majukumu yao
watashirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wanaohusika na chaguzi ukiwemo
uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi mkuu mwaka 2020.
Muungano huo umezinduliwa leo Novemba 1,
mwaka 2019 jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine viongozi wake
wameeleza kuwa malengo yao, matarajio yao na ushiriki wao katika kujadili
mafanikio na changamoto zilizopo katika michakato mbalilmbali ya uchaguzi.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa ACHA Martina Kabisama amesema wameona iko haja ya wao
kuunganisha nguvu ya pamoja na kufanya kazi
zinazohusiana na uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2019 na
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
"Naomba nieleweke vizuri
vibali ambavyo tumevipata ni kwa ajili ya kutoa elimu ya uraia pamoja na ile ya
mpiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi
mkuu mwaka 2020,"amesema Kabisama
na kuongeza muungano huo upo kihalali kwani umefuata tararibu zote na hata
asasi zilizounda muugano huo zimesajiliwa na zinatambuliwa kisheria.
Amefafanua zaidi wameamua kuwa na muungano
huo baada ya kuona ndani yao wamo wabobezi wa masuala ya uchaguzi ambapo
waliangalia kabla ya kufikia uamuzi huo waliangalia masuala ya uchaguzi na
ushiriki wa wananchi na kubaini wanayo nafasi ya wao kuunganisha nguvu ili
chaguzi ziwe na mafanikio kabla na baada ya chaguzi.
"Katika kufuatilia tulibaini kuna
mafanikio makubwa katika chaguzi zetu na wakati huo huo kuna changamoto, hivyo
tumeona tuje na huu muunganiko kwa ajili ya uchaguzi kwani hakuna sababu ya
sisi kubaki nyuma lazima tushiriki ili tuwe sehemu ya kuondoa changamoto
zilizopo.
"Katika changamoto hizo zinaweza kuwa zinazohusu wananchi, sheria au
vyombo vinavyosimamia uchaguzi aidha wa
Serikali za Mitaa au Uchaguzi Mkuu .Hivyo lazima tukae na kutafuta
ufumbuzi kwa pamoja,"amesema.
Hata hivyo amesema katika kuhakikisha
muungano huo unakwenda vizuri waliamua kujiwekea malengo yao kwani kuungana
bila kuwa a malengo ni rahisi kuvunjika. Ametumia nafasi hiyo kueleza taasisi
za chaguzi zipo na zinapita katika michakato
mbalimbali hadi inapofikia hatua ya kupiga kura na kisha kuingia katika
mchakato wa kuanza uchaguzi mwingine.
"Uchaguzi ni kama duara, tunapomaliza
uchaguzi mmoja tunaanza safari ya uchaguzi mwingine.Hivyo muungano wetu nao
tutashiriki kikamilifu Uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2019 na baada ya
hapo tutaendelea na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020,"amesema .
Ameongeza taasisi ambazo zinahusika na chaguzi za
Serikali za Mitaa ni Wizara ya Nchi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa(TAMISEMI) , hivyo ameahidi kushirikina na TAMISEMI
kuhakikisha uchaguzi huo wa mitaa unakwenda vizuri na katika uchaguzi mkuu mwaka 2020
watashirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Zanzibar(ZEC).
Wakati huo huo Kabisama amezungumzia umuhimu
wa Watanzania kushiriki katika chaguzi huku wakihakikisha nchi inaendelea kuwa
na amani na usalama na kuongeza wajibu wa kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga
kura kujiandikisha na siku ya kupiga kura anakwenda kuchagua kiongozi au
viongozi kwa maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ACHA Justina
Shauri amesema vyombo vya habari vinadhamana kubwa ya kufikisha taarifa na
hivyo wanategemewa sana katika kufikisha habari zinazohusu elimu kwa mpiga kura
na mchakato wa kupiga kura.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Shauri
amesisitiza umuhimu wa uhuru wa demokrasia kwa kuhakikisha watu wanaachwa wafanya
kazi za uchaguzi kwa mujibu wa sheria na kama watu wanataka kuundamana basi taratibu
zifuatwe.
Pia Shauri amezungumzia suala la uangalizi
wa ambapo katika hilo amesema waangalizi wa uchaguzi wanapaswa kutekeleza
majukumu yao na hiyo itasaidia kutambua changamoto zilizopo na hatimaye
zitapatiwa ufumbuzi.
"Ukiwa makini katika suala la uangalizi
wa uchaguzi kuna mambo tu utayabaini aidha ya mafanikio au changamoto.Hivyo
itakuwa rahisi kuboresha chaguzi zetu maana yale ambayo yatakuwa kama sababu za
kukwamisha mchakato yatapata ufumbuzi,"amesema Shauri na kuongeza hivyo
moja ya majukumu yao ni kutoa elimu pia kwa waangalizi nini wafanye ili kazi
hiyo kufanyika kwa ufasaha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...