Veronica Simba – Dodoma
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, amezindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na kuitaka kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni.
Tukio hilo lilifanyika Novemba 4, 2019 katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati zilizopo Kikuyu, Dodoma na kushuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt Hamisi Mwinyimvua na viongozi wengine wa Wizara, ambapo Waziri alimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi husika, Dkt Lutengano Mwakahesya, Kanuni zitakazomwongoza yeyé na Wajumbe wa Bodi, katika kutekeleza majukumu yao.
“Nakukabidhi Kanuni mtakazotumia kutekeleza majukumu yenu ili kazi zenu zikawe zenye ufanisi. Fanyeni kazi zenu zote kwa kuzingatia sheria na kanuni.”
Akizungumzia majukumu makuu ya Bodi hiyo, Waziri Kalemani alisema jukumu kubwa ni kuhakikisha shughuli za kuingiza mafuta kwa pamoja zinaratibiwa ipasavyo ili yapatikane kwa muda wote.
“Mnatakiwa kuhakikisha uratibu unakuwa ni sahihi, usiosababisha migogoro kati ya waagizaji wa mafuta kwa pamoja na watoa huduma wengine,” alisisitiza.
Vilevile, Waziri alieleza jukumu lingine ni kwa Bodi kuhakikisha kuwa mafuta yanayopatikana yana viwango vinavyokidhi ubora na mahitaji ya sekta ya mafuta hapa nchini.
Katika hatua nyingine, Waziri alielezea hali ya upatikanaji mafuta nchini, ambapo alisema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, hali hiyo imeimarika kwa kiasi kikubwa.
Akitoa takwimu, Waziri alisema hadi kufikia mwaka 2015, nchi ilikuwa na Bandari moja tu ya Dar es Salaam iliyokuwa na uwezo wa kupokea Meli za Mafuta tani 165,000. “Sasa zimeongezeka Bandari mbili, Mtwara na Tanga, zenye uwezo wa kupokea mafuta tani 90,000 hivyo uwezo wetu wa jumla wa kupokea mafuta kwa sasa ni tani 255,000.”
Waziri aliendelea kueleza kuwa, uwezo wa nchi kuingiza mafuta kwa sasa ni lita milioni 265 kwa siku wakati mahitaji ni lita milioni 9.4 tu. “Hivyo tuna ziada ya lita milioni 255.3 kwa siku.”
Akidadavua zaidi, Waziri alieleza kuwa, nchi ina ziada ya mafuta ya dizeli kiasi cha lita milioni 151.2 ambazo zinatosha kwa matumizi ya siku 32; aidha, kuna ziada ya lita milioni 85.3 za petroli ambazo zinatosha kwa matumizi ya siku 26.
Kwa upande wa mafuta ya ndege, alisema kuwa, ipo ziada ya lita milioni 22.9 ambazo zinatosha kwa siku 41 na ziada ya lita milioni 5.7 za mafuta ya taa ambayo yanatosheleza mahitaji ya siku 40.
Hata hivyo, Waziri alibainisha kuwa, katika kipindi cha miaka minne, mahitaji ya mafuta ya taa kwa nchi yamepungua kutokana na kuenea kwa umeme katika maeneo mengi.
Alisema, takwimu zinaonesha mwaka 2015 mahitaji ya mafuta ya taa kwa siku yalikuwa lita 1,070,000 ambapo yamepungua hadi kufikia lita 1,045,000 kwa siku kwa sasa.
Waziri Kalemani alitumia jukwaa hilo kutoa onyo kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa na tabia ya kuficha mafuta wakisubiri bei ipande ndipo wayatoe na kuuza. Aliitaka Bodi kuwafikishia salamu kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria na atakayekamatwa atachukuliwa hatua kali ikiwemo kufungiwa kituo chake.
Waziri pia, alitoa maelekezo kwa Bodi hiyo kufanyia kazi suala la kuhakikisha wananchi wa vijijini wanaondokana na changamoto ya upatikanaji wa mafuta. Aliwataka kufanya mazungumzo na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ili wafanye tathmini itakayowezesha uanzishwaji wa vituo vya kuuzia mafuta vijijini.
Alisema, wananchi vijijini wamekuwa wakihangaika kupata mafuta na wakilazimika kununua nishati hiyo kwenye madumu kutoka kwa wauzaji holela mabarabarani jambo ambalo siyo salama.
“Tunavyopeleka umeme vijijini, tupeleke pia na mafuta ili kuwaondolea adha wananchi. Hii itawasaidia sana wahitaji, hususan wamiliki wa taxi, bodaboda na bajaji,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Mwinyimvua, pamoja na kuwapongeza wajumbe wa Bodi kwa kuteuliwa kwao, aliwataka pia kufanya kazi kwa bidii na kutimiza majukumu yao kama alivyoelekeza Waziri.
Naye Mwenyekiti wa Bodi, aliahidi kwa niaba ya wenzake kuwa watafanyia kazi yale yote waliyoelekezwa.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kulia), akimkabidhi Kanuni za Kazi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Dkt Lutengano Mwakahesya (kushoto). Anayeshuhudia (katikati) ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua. Waziri aliizindua rasmi Bodi hiyo Novemba 4, 2019 jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia), akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) (hawapo pichani), wakati alipokuwa akiizindua rasmi Bodi hiyo Novemba 4, 2019 jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (Meza Kuu-kulia), akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) (kushoto), wakati alipokuwa akiizindua rasmi Bodi hiyo Novemba 4, 2019 jijini Dodoma. Kulia kwa Waziri ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua na walioketi upande wa kulia ni viongozi mbalimbali wa Wizara pamoja na wataalamu kutoka Wakala hiyo.
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akiizindua rasmi Bodi hiyo, Novemba 4, 2019 jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), baada ya kuizindua rasmi Bodi hiyo Novemba 4, 2019 jijini Dodoma. Kushoto kwa Waziri ni Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Hamisi Mwinyimvua na kulia kwa Waziri ni Mwenyekiti wa Bodi husika, Dkt Lutengano Mwakahesya.
Baadhi ya viongozi wa Wizara ya Nishati wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Novemba 4, 2019 jijini Dodoma. Kutoka kushoto ni Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi; Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Raphael Nombo na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Maseke Mabiki.
Baadhi ya wafanyakazi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala huo, Novemba 4, 2019 jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...