-KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao akizungumza na Vyombo vya Habari.
 
 NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimetaka Chama cha ACT-Wazalendo kuacha siasa za kishamba zilizopitwa na wakati ambazo zinalenga kuhatarisha amani ya nchi.

Kimesema Viongozi wa ACT-Wazalendo wameendelea na mikakati michafu ya kujitafutia umaarufu na huruma ya kisiasa kupitia matamshi yenye uchochezi,kashifa,dharau na upotoshaji dhidi ya viongozi wa Serikali na CCM.

Akizungumza Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Catherine Peter Nao, amesema CCM haitovumilia mwenendo wa siasa za maji taka za kuwatukana na kuwadhalilisha Viongozi wa Serikali na Chama hicho zinazofanywa na ACT-Wazalendo.

Catherine, ameendelea kuvitaka vyombo vya dola nchini kuchukua hatua za haraka dhidi ya wanasiasa hao wanaotumia vibaya uhuru wa kisiasa kwa kuwadhalilisha viongozi wa umma.

"Siku za hivi karibuni tumeona namna viongozi ACT-Wazalendo walivyomtukana Naibu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.Mhandisi Hamad Yussuf Masauni mitandaoni na Jeshi la Polisi lipo na halijachukua hatua stahiki.

Wenzetu hao baada ya kushindana kwa hoja na kufanya kazi za Wananchi wao wanakuja na mtindo wa matusi sasa tunawaonya na wasipoacha tabia hiyo wajue ushahidi wa maovu yao tunao na tutawafikisha kwenye vyombo vya sheria.", alisema Catherine Peter nao.

Kupitia mkutano huo Catherine alilaani hatua ya upotoshwaji unaofanywa na chama cha ACT-Wazalendo kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura ambalo linatarajia kuanza uandikishwaji visiwani hapa Januari 18 hadi Machi 4 mwaka 2020.

Alisema mchakato huo wa kikatiba na kidemokrasia wa uandikishaji wa daftari hilo umeanza kuchafuliwa kwa hoja dhaifu na wanasiasa wanaoweka mbele maslahi yao badala ya maslahi ya nchi.

Aliongeza kuwa mshakato huo ndio chimbuko la uwepo wa uchaguzi mkuu ujao hivyo panahitajika ustaarabu kwa vyama vyote vya kisiasa nchini.

Katibu huyo Catherine alisema kinachofanywa na ACT-Wazalendo ni kuleta hofu kwa wananchi na kukwamisha ukamilishaji wa uandikishwaji wa daftari la wapiga kura ambapo jambo hilo lipo kwa mujibu wa sheria.

"Tunahitaji siasa za kistarabu pamoja na mchakato huu ambao unaanza wa uandikishwaji wa daftari hilo la wapiga kura hivi karibuni ufanyike kistaarabu na hakuna sababu ya kuwepo kwa hali ya uvunjifu waamani,"alisema.

Catherine alisema CCM haifanyi kazi ya uandaaji wa vitambulisho bali inafanya kazi za siasa na kwamba katika ofisi ya chama hakuna kitu kama hicho ambacho ACT-Wazalendo wanadai shutuma hizo.

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Kamati ya Itikadi,Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Salim Abdallah Bimani alishutumu kuwa CCM imeandaa njama za kuwaandikisha vijana ambao hawajatimia umri wa kupiga kura lengo likiwa kuongeza idadi ya kura kwa Chama.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...