Wataalam wa chumba cha upasuaji kituo cha afya Kome wakiwa kwenye chumba hicho.
*************************
Na.Catherine Sungura
Kituo cha afya Kome kilichopo
halmashauri ya buchosa wilayani Sengerema kimefanikiwa kufanya upasuaji
wa kwanza wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni na hivyo kumuokoa mama na
mtoto wake.
Akiandika kwenye mtandao wa
kijamii Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy
Mwalimu amesema kuwa kwa mara ya kwanza kituo hicho kimeweza kufanya
upasuaji huo baada ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kujenga “theatre” na
kuweka vifaa tiba kwenye kituo hicho.
Waziri Ummy ameendelea kuandika
kuwa chumba hicho cha upasuaji ambacho kipo kituoni hapo kitawasaidia
akina mama wajawazito wa kisiwa cha kome watakaopata uzazi pingamizi na
hivyo kutokufuata huduma hizo wilayani sengerema na hivyo kutokuvuka
tena maji.
“Hakika tumedhamiria kuokoa
maisha ya akina mama wajawazito na watoto wachanga,tutaendelea kuchukua
hatua ili kuhakikisha huduma za uzazi za dharura ikiwemo ya upasuaji
wa kumtoa mtoto tumboni(CEmONC) zinapatikana katika vituo vyote vya afya
vya umma ,mama na mtoto huyo mwenye uzito wa kilo 3 na nusu wanaendelea
vizuri”Amesema waziri Ummy
Naye Mganga Mkuu wa halmashauri
ya buchosha Dkt. Ernest Chacha amesema walimpokea mama huyo kituoni hapo
siku ya ijumaa ambaye alikua akihudhuria kliniki kwenye zahanati moja
huko kisiwani hakuweza kujifungua kawaida kwani alikua akikabiliwa na
uchungu pingamizi kwani nyonga zake hazikuwa zinapanuka hivyo ili
kumuokoa ilibidi afanyiwe upasuaji kuweza kumuokoa mama pamoja na mtoto .
Dkt. Chacha ameishukuru Serikali
ya awamu ya tano kwa uboreshaji wa vituo vya afya nchini ikiwemo kituo
cha afya cha kome ambacho kipo kisiwani kwa kuboresha miundombinu kwa
kujengewa chumba cha upasuaji pamoja na kuwekewa vifaa tiba hivyo
kusaidia kuokoa maisha ya akina mama wajawazito na watoto wachanga
hususan visiwani humo.
“Wananchi walikua wanapata adha
kubwa sana ya kuvuka maji kutoka kisiwani na kufuata huduma kwenye
hospitali ya wilaya iliyopo sengerema,tunamshukuru Waziri Ummy Mwalimu
kwa kuiagiza MSD kutufungia taa kwenye chumba cha upasuaji wakati wa
ziara yake hivi karibuni visiwani hapa kwani tumeweza kuokoa maisha ya
huyu mama muda mfupi baada ya taa hizo kufungwa”Amesema Dkt. chacha
Hivi karibu waziri wa afya
alitembelea kisiwa hicho na kuwaahidi kuwapatia xray mashine ya
kidigitali kwenye kituo hicho cha afya na kuwataka MSD kufunga taa
kwenye chumba hicho cha upasuaji mara moja.
Kisiwa cha kome kimeongeza
idadi ya akina mama wanaojifungulia kwenye vituo vya afya kwa
asilimia 80 kwa mwaka ambapo wastani akina mama 50 wanajifungulia kwa
mwezi
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...