Baadhi ya abiria wakipakia mizigo katika boti za abiria katika Bandari ya Magarini wilayani Muleba mkoani Kagera.Bandari hiyo imeboreshwa kwa kujengwa kwa miundombinu yake ikiwemo majengo ya ofisi, vyoo na gati kwa ajili ya meli na boti kuegesha bandarini hapo.
Baadhi ya abiria wakiingia ndani ya boti ya abiria kabla ya kuanza kwa safari kutoka Bandari ya Magarini kuelekea katika visiwa vingine vilivyomo katika Ziwa Victoria.
Abiria wakiwa wamekaa ndani ya boti kwa ajili ya kuanza safari katika bandari ya Magarini.
Mmoja wa wakazi wa Muleba akiwa katika bandari ya Magarini (aliyenyoosha vidole) akiwa amezungukwa na baadhi ya waandishi wa habari waliofika bandarini hapo kuangalia uboreshwaji wa miundombinu katka bandari hiyo.
moja wa wananchi akielekea kupanda boti ya abiria katika bandari ya Magarini wilayani Muleba mkoani Kagera.
Boti ya abiria ikiwa imeegesha ikisubiri kuanza kupakia abiria katika Bandari ya Magarini wilayani Muleba mkoani Kagera.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Muleba
WANANCHI wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera na hasa wanaoutumia usafiri wa meli na boti za abiria kufanya safari zao mbalimbali katika Visiwa vilivyomo ndani ya Ziwa Victoria wameipongeza Serikali Kuu na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) kwa hatua yake ya kuboresha miundombinu ya Bandari ya Magarini ambayo sasa imekamilika.
Wakizungumza na Michuzi Globu ya Jamii pamoja na Michuzi TV, wananchi hao wamesema kuwa hakika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli kupitia TPA umeonesha namna ambavyo umedhamiria kuboresha maisha ya watu kwa kuhakikisha huduma muhimu zinapewa kipaumebele na kwamba wao miundombinu ya bandari katika Ziwa Victoria ni muhimu kwani ndio njia rahisi ya kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Akizungumza leo kuhusu bandari ya Magarini, Mkazi wa eneo hilo Paul Stephen amesema kuwa wanathamini kazi inayofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari katika kuboresha miundombinu ya bandari hiyo ambayo kabla ya uboreshwaji wa miundombinu wananchi walikuwa wanapata huduma ya usafiri wa boti za abiria katika mazingira magumu.
"Tunatoa shukrani kwa Serikali pamoja na Mamlaka ya Bandari kwa hatua hii iliyochukua ya kuboresha majengo , gati na ofisi za Bandari ya Magarini ambayo kwetu ni muhimu katika shughuli za kiuchumi.Tunaitegemea sana kwani ndio ambayo tunaitumia tunapotaka kufanya safari zetu za kila siku.Kwa uboreshaji wa miundombinu ambao umefanyika, tutaona manufaa yake na itakuwa chachu ya maendeleo kwetu,"amesema Stephen.
Wakazi wengine wa eneo hilo wametoa ombi kuhusu kuangaliwa upya kwa ushuru ambapo walisema wanalipa Sh.600 wakati katika maeneo mengine bei ya ushuru kwa kila abiria ni Sh.200 au Sh.400.Hivyo ni matarajio yao Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari itasikia kilio chao kwa kushusha gharama za ushuru.
Hata hivyo Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari katika Bandari za Ziwa Victoria Morric Mchindiuza amesema kuwa amesikia maombi ya wananchi hao kuhusu bei ya ushuru.Amesema kuwa katika bandari zote nchini gharama ya ushuru kwa kila abiria ni Sh.600 na kinachotokea kuna bandari bubu ambazo zenyewe zinatoza bei ya Sh.200 hadi Sh.400.
"Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, tunao utaratibu ambao unatambulika kisheria kuhusu ushuru na tozo nyingine.Hili la ushuru wa abiria bandari zote nchini bei yake ni moja na hivyo kinachosemwa na wananchi ni ushauri ambao tumeuchukua na tutaufanyia kazi.Hata hivyo kama ambavyo tumekuwa tukielekeza kila siku bandari bubu zinakwenda mwishoni , hivyo bei ya ushuru itabaki ile inayotambuliwa na TPA,"amesema Mchindiuza wakati anafafanua kuhusu gharama za ushuru bandarini.
Kuhusu bandari hiyo ya Magarini amesema kuwa kwa sasa ujenzi wa miundombinu umekamilika kwa asilimia kubwa na kilichobaki ni kuanza kutumika rasmi kwa majengo ya bandari hizo ingawa kwa upande wa gati imeanza kutumika.
"Tumejipanga kuhakikisha tunaboresha miundombinu ya bandari zetu za Ziwa Victoria na ndio maana kila mahali ambapo tunakwenda utakuta aidha ujenzi umekamilika au unaendelea na mkakati wetu ni kuhakikisha usafiri wa meli unakuwa wa uhakika ili wananchi sasa waweze kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine,"amesema Meneja huyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...