Waziri wa Madini Doto Biteko,
akiongea na Wafanyabiashara ya Madini katika Mkutano uliofanyika katika
Ukumbi wa Mount Meru jijini Arusha

Waziri wa Madini Doto Biteko
(katikati), akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo (kulia), na
(kushoto) ni Mwenyekiti wa Tume ya Madini Pro. Idris Kikula wakijadili
jambo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Waziri wa Madini Doto Biteko
watatu kutoka Kushoto, kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) Mkoa wa Arusha, Zelothe Steven Zelothe na wapili kutoka kushoto
ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo

Baadhi ya Wafanyabiashara wa Madini wakiwa kwenye Soko la Madini jijini Arusha.

Waziri wa Madini Doto Biteko
(kulia) akiwa na Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Watu Wenye Ulemavu, Anthony Mavunde (katikati) na kushoto ni Kamishna wa
Madini, David Mulabwa

Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa
na baadhi ya viongozi walioshiriki Mkutano wa Waziri wa Madini na
Wafanyabiashara ya Madini jijini Arusha.
……………
Na Tito Mselem,Arusha
Waziri wa Madini Doto Biteko
amewataka wafanyabiashara wa Madini ya Vito kote nchini kuhakikisha
wanafanya biashara zao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu
zilizowekwa na Serikali.
Waziri Biteko ameyasema hayo
Desemba 21, 2019 wakati akizungumza na Wafanyabiashara wa Madini
(Dealers na Brokers) kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Mount
Meru, jijini Arusha.
Waziri Biteko
amewatahadharisha wafanyabiashara wote kwamba, wale wote wanaofanya
vitendo vilivyo kinyume na taratibu zilizowekwa na serikali
watachukuliwa hatua kali za kisheria. Pamoja na mambo mengine,
Waziri Biteko amesisitiza suala la Sheria na Kanuni zinazohusu masoko na
uongezaji thamani wa madini ya vito pamoja na masharti ya leseni
wanazomiliki.
“Nipende kueleza kwamba, wale
wote wanaofanya biashara ya madini kwa kufuata Sheria na Taratibu
hawatabuguziwa na mtu yoyote, hivyo niwaombe wadau wote waa madini
kufuata taratibu”, Waziri Biteko alisema.
Wakati huo huo, Waziri Biteko,
amevitaka vyama vyote vya madini nchini kushirikiana na kupendana
katika biashara ya madini na kueleza, kwamba, kwenye biashara ya madini
kuna majungu mengi ambayo hayana tija.
Aidha, Waziri Biteko
amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri wanazozifanya
katika kusimamia na kulinda rasilimali madini nchini.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anawapenda sana wafanyabiashara na
wachimbaji wa madini lakini anachukizwa sana akisikia kwamba kuna mtu
amekamatwa akitorosha madini au anakwepa kodi ya serikali,” alisema
Waziri Biteko.
Awali, Waziri Biteko alitembelea
soko la Madini la jijini Arusha na kuwapongeza wafanyabiashara wote wa
madini kwa kufuata agizo la serikali la kuhamishia shughuli za madini
katika soko hilo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu
Wenye Ulemavu, Anthony Mavunde, amesema Nchi inawahitaji wataalamu wa
madini kwa asilimia kubwa na kuanzia mwakani Wizara yake itaanza kuweka
mikakati ya upatikanaji wa vibali vya ajira kwa wageni kwa haraka.
Nae, Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Mrisho Gambo, amempongeza Waziri wa Madini Doto Biteko, kwa usimamizi
mzuri wa Rasilimali Madini nchini na juhudi kubwa anazo zifanya katika
kutatua changamoto wanazozipitia wafanyabiashara na wachimbaji wa madini
nchini.
“Nichukue fursa hii, kuwataka
wadau wote wa madini nchini kumuunga mkono Waziri wa Madini kwa kufuata
Sheria naTaratibu zilizowekwa na serikali na kuachana na suala la
kutorosha madini,” Gambo alisema.
Pia, Mwenyekititi wa Tume ya
Madini, Prof. Idris Kikula, amesema Tume ya Madini imejipanga kikamilifu
kuhakikisha leseni zinatolewa kwa wakati kwa waombaji na kuimarisha
usimamizi wa Masoko ya Madini nchini.
Nae, Mkurugenzi wa Huduma za
Sheria wa Wizara ya Madini, Edwin Igenge ameeleza kwamba Sheria ya
Madini ya Mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 inatoa mwongozo
kwa shughuli zote za madini nchini na kuwataka wadau wote wa madini
kusoma Sheria mpya ya madini ili waelewe miko na taratibu za shughuli
hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...