Kivuko kipya cha MV.Ilemela
kikielea majini mara baada ya kushushwa , kivuko hicho ambacho ujenzi
wake umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.7 za Kitanzania kitakua
kikitoa huduma kati ya Kayenze na Kisiwa cha Bezi na kina uwezo wa
kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100.

Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi
na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano) Mhe. Atashasta Nditiye
katikati akiwa ameshikana mkono na Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella
katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza zoezi za kushusha kivuko
kipya cha Kayenze na kisiwa cha Bezi kilichogharimu shilingi bilioni 2.7
ambacho kimepewa jina MV.Ilemela, tukio lililofanyika katika yadi ya
Songoro Ilemela jijini Mwanza. Kushoto kwa Mongella ni Mbunge wa
Iilemela Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi Mhe. Angelina Mabula na
wa tatu kushoto ni Mtendaji Mkuu TEMESA Mhandisi Japhet Maselle. Kivuko
cha MV.Ilemela kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani
100.

Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi
na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano) Mhe. Atashasta
Nditiye katikati akifurahia jambo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle wa pili kushoto mara baada ya
kumaliza zoezi la kukagua na kukishusha kwenye maji kivuko cha
MV.Ilemela. Kivuko cha MV.Ilemela kina uwezo wa kubeba abiria 200 na
magari 10 sawa na tani 100 na kimejengwa kwa gharama ya shilingi
bilioni2.7.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle akisoma taarifa fupi ya mradi
wa ujenzi wa kivuko cha MV.Ilemela wakati wa hafla ya kukishusha majini
kivuko hicho iliyofanyika katika yadi ya Songoro iliyopo Ilemela jijini
Mwanza. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella na katikati ni
Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na
Mawasiliano) Mhe. Atashasta Nditiye. Kivuko cha MV.Ilemela kina uwezo
wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100 na kimejengwa kwa
gharama ya shilingi bilioni2.7.
…………………………………………………
NA ALFRED MGWENO (TEMESA MWANZA)
Wakazi wa Ilemela mkoa wa Mwanza
leo wameshuhudia kwa mara ya kwanza kivuko kipya cha Kayenze Bezi,
MV.Ilemela ambacho kimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.7
kikishushwa kwenye maji baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Tukio hilo
limefanyika katika yadi ya Songoro iliyopo Wilaya ya Ilemela ambapo
mgeni rasmi alikua Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
(Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano) Mhe. Atashasta J. Nditiye (MB).
Akizungumza katika tukio hilo
Mhe. Nditiye alimshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya awamu ya tano kwa
kuendelea kutimiza ahadi ya miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
‘’Hadi sasa Mheshimiwa Rais
tayari ameshatoa fedha zote kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni
9,953,916,200 iliyokuwa imepangwa kwenye bajeti ya miradi ya maendeleo
ya vivuko kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020’’, alisema Mhe. Naibu Waziri
ambapo aliongeza kuwa kivuko cha MV.Ilemela kitakapoanza kutoa huduma
kitaondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi kati ya Kayenze na kisiwa
cha Bezi.
‘’Kivuko hiki kitakapoanza kutoa
huduma ni dhahiri kuwa kitaondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi kati
ya Kayenze na kisiwa cha Bezi hivyo kitainua maisha ya wananchi wa
maeneo hayo kibiashara, kiuchumi na kijamii, mara tu mtakapokamilisha
majaribio anzeni kutoa huduma ’’. Aliongeza Naibu Waziri ambapo pia
alitoa wito kwa watumishi wa TEMESA kufanya kazi kwa weledi na
kuhakikisha kivuko hicho pamoja na vivuko vingine vinatunzwa vizuri na
vinadumu kwa muda mrefu huku wakizingatia usalama wa abiria na mali zao.
Awali, Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, akisoma
taarifa kwa mgeni rasmi katika tukio hilo alisema serikali kupitia
TEMESA inaendelea na ujenzi wa vivuko vingine vipya kwa ajili ya Mafia
Nyamisati kwa gharama ya shilingi bilioni 5.3, Bugorola Ukara kwa
gharama ya shilingi bilioni 4.2 pamoja na Chato Nkome kwa gharama ya
shilingi bilioni 3.1.
‘’Vivuko hivi vyote vinagharimu
jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 15.3 na fedha zote hizi
zinatolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’, alisema
Mhandisi Maselle ambapo aliishukuru serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha
zote zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ununuzi wa vivuko,
ukarabati na ujenzi wa maegesho ya vivuko, ambapo alisema Fedha hizo
zimewezesha miradi hiyo kuanza na mingine kuwepo katika hatua mbalimbali
za utekelezaji.
Naye Mbunge wa Ilemela Mhe. Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula
akizungumza katika tukio hilo aliishukuru serikali kwa kuweza kutimiza
ahadi iliyoitoa. ‘’Nimshukuru Mhe. Rais niwashukuru TEMESA kwa kazi
kubwa na nzuri ambayo imefanyika, tunao uhakika sasa kwamba adha ya
usafiri katika eneo la visiwa vya Kayenze Bezi sasa litakua ni
historia’’, alisema Dkt. Mabula.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John
Mongella alimuomba Mhe. Nditiye kufikisha salamu za shukrani kwa Rais
kwa mambo makubwa anayoufanyia mkoa wa Mwanza hasa kwenye sekta ya
usafiri wa majini ambapo alisema watu wa mkoa huo wanategemea mwezi wa
pili kuona vivuko vingine vikiingia ziwani tayari kuanza kutoa huduma
kwa wananchi.
Kivuko cha MV.Ilemela kina uwezo
wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100. Hadi sasa Wakala
unaendesha na kusimamia vivuko 30 katika vituo (Ferry stations) 20
Tanzania Bara na hivyo kukamilika kwa kivuko cha MV. Ilemela kutafanya
idadi ya vivuko kufikia 31 na vituo kuwa 21.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...