WAKATI zoezi la undikishaji kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapiga kura likianza mkoani Ruvuma,baadhi  ya wananchi wa Mji wa Mbinga,wameipongeza Serikali kupitia tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) kuanza zoezi hilo mapema kwa kile walichodai litatoa fursa kwa baadhi yao kushiriki katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana,wananchi hao Angelus Kapinga na John Kowelo wamesema, uamuzi wa uliofanywa na Tume hiyo kuanza mchakato  wa uandikishaji  na maboresho katika Daftari la kudumu la wapiga kura, ni ishara njema kwamba uchaguzi Mkuu  ujao utakuwa huru na haki na Watanzania wengi watashiriki kuchagua viongozi wao kwa kuwa wengi watajiandikisha.

Angelus Kapinga alisema, yeye binafsi anafurahi kuona uchaguzi Mkuu wa mwaka huu atatumia haki yake ya msingi kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi kuanzia  nafasi ya Udiwani,Ubunge na Rais kwa sababu katika uchaguzi  wa Mwaka 2015  hakufanikiwa kupiga kura kwani alikuwa na umri chini ya miaka 18 ambao hauruhusiwi kisheria kupiga kura.

John Kowelo amepongeza uhamasishaji mkubwa unaofanywa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbinga mjini  Grace Quintine, namna alivyojipanga kuhakikisha wananchi wenye sifa wanapata haki yao kujiandikisha katika Daftari la kudumu  la Wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Mwezi Oktoba.

Alisema, Quintine ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mj Mbinga anapita kila mtaa  na ma gari yenye vipaza sauti na wakati mwingine kwa miguu  kuhamasisha kujitokeza katika vituo vya kujiandikisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura, jambo linaloonekana kuwavutia watu wengi  wa Mji wa Mbinga.

Kwa upande wake,msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbinga mjini Grace Quintine amewataka waandikishaji wasaidizi wa Daftari la kudumu la wapiga kura kuwa makini,kuzingatia sheria na kanuni za Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wote wa zoezi la Undikishaji wa wananchi katika Daftari la wapiga kura.

Amewataka  waandishi hao, kuhakikisha wakati wote wanakuwa  vituoni ili kuepuka usumbufu kwa wananchi wanaokwenda kujiandikisha.

Pia amewakumbusha kwenda kushirikiana na wadau wengine wakiwemo mawakala wa vyama vya siasa  kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la  kudumu la wapiga kura katika maeneo yao.

Quintine ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mbinga,amewataka waandishi  kutumia muda wa ziada kusoma kwa makini maelekezo yote waliyopewa wakati wa semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo ili kazi zao watekeleze kwa weledi.

Mbali na maagizo hayo,amewataka waandishi hao kutunza vifaa walivyopewa na Tume na kuhakikisha kila mtu mwenye sifa anayestahili kuandikishwa katika Daftari hilo anaandikishwa  kama atakuwa na sifa.

Aidha, amewaonya kujiepusha kufanya kazi  kwa miemko ya kisiasa  na kwamba, Serikali inawaamini  watatekeleza vema majukumu  waliyopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

“mkafanye kazi zenu kwa kufuata na kuzingatia sheria na taratibu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi,shirikianeni na wadau wakiwemo mawakala wa vyama vya Siasa kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la kudumu la Wapiga kura,mjiepushe sana Itikadi za Vyama,mmekula kiapo kwa ajili ya kuwatumikia watu wote” alisema Quintine.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...