Meneja wa Kampuni ya LAMBOKILE Stephen Mliga (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mchakato wa tuzo za FISA zinazotarajiwa kutolewa hivi karibuni ambapo amesema kuwa vijana 53 wameingia katika hatua za mwisho za kinyang'anyiro hicho, kulia ni Meneja Mradi wa Tuzo za FISA Jacob Tito na kushoto ni Mratibu wa tuzo hizo James Chitemo, leo jijini Dar es Salaam.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

KAMPUNI ya Lambokile inayojishughulisha na utatuzi wa changamoto za kibiashara kwa vijana wa kitanzania pamoja na wajasiriamali imewataja vijana 53 walioingia katika hatua ya mwisho ya kinyang’anyiro cha tuzo 20 zilizokwenda na kauli mbiu ya "Kesho Niitakayo" yaani FISA;  (The Future I Want Awards) ambapo washindi hao wamepatikana kati ya vijana 418 waliokuwa wamewania tuzo hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Meneja wa Kampuni hiyo Stephen Mliga amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikitoa mchango mkubwa kwenye Sekta ya biashara hasa kwa vijana kupitia miradi yake mikubwa mitatu ukiwemo wa Kesho Niitakayo (The Future I Want) na ule wa Mtaani Fund.

“Nipende kusema kuwa mbali na hiyo miradi miwili, pia tunao mradi mwingine wa tatu unaojulikana kama; Anzisha na Boresha Biashara yako (SIYB) Mradi ambao umejikita katika kusaidia watu katika kuendesha biashara zenye tija na hiyo ni pamoja na kutengeneza wazo bora la biashara, kuanzisha biashara yenyewe pamoja na  kuiboresha na kuikuza" amesema Mliga.

Amesema kuwa vijana ni kundi kubwa ambalo linahitaji kuwezeshwa  ili kuweza kujenga uchumi imara wa taifa na hiyo ni pamoja na kwenda sambamba na Serikali ya awamu ya tano ambayo imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa tuzo za FISA Jacob Tito, amesema kuwa kikao hicho na waandishi wa habari kimekuwa ni sehemu ya kutoa mrejesho juu ya mlolongo wa tuzo husika pamoja na vijana walioibuka kidedea na kuingia tatu bora katika kila kipengele cha kinyanganyiro cha tuzo hizo na watapata nafasi ya kujieleza mbele ya majaji siku ya utoaji wa tuzo husika.

“Awali tulianza na vijana 418 walioomba na kupendekezwa badaye tukafanya mchujo kwa kuzingatia ubunifu, uthubutu wa washiriki pamoja na matokeo chanya kwenye jamii nzima ambapo tuliweza kuwapata washiriki 70 waliopigiwa kura na badaye tuliendelea na mchakato ambapo leo ndio tumewatangaza hawa 53 waliofuzu kuingia hatua ya mwisho,”amesema Meneja Tito.

Tito amesema kuwa vijana wana bunifu nyingi ambapo zikitumiwa zitaleta matokeo chanya katika jamii na kushauri kuwa Serikali kwa kushirikiana na asasi za kiraia ikiwemo LAMBOKILE ziwe sehemu ya kuwainua na kuwawezesha.

Vilevile Mratibu wa Tuzo hizo James Chitemo, amesema mchakato kuwapata vijana hao 53 ulikuwa  mgumu na wenye ushindani mkubwa sana kwani vijana 418 waliogombea walitokana na mapendekezo kutoka kwa vijana 268 na waliojipendekeza wenyewe walikuwa 150.

“Watu 6551 walishiriki kuwapigia kura  watu wanne katika kila kipengele ili kuwapata tatu bora ambao wameingia katika kinyang’anyiro hiki ambapo mgawanyo wa kura pamoja na asilimia walizopata washindi zinapatikana katika mitandao ya kijamii pamoja na tovuti zetu." amesema.

 Chitemo, amesema kuwa lengo la kura ilikuwa ni ushirikishwaji na utoaji fursa kwa umma kuchagua washiriki halali watakaoingia kwenye kinyang’anyiro cha tatu bora kama walivyopatikana na kuwatangaza.

Aidha, amesema, pamoja na  kukumbana na changamoto mbalimbali lakini kuna baadhi ya mambo ya msingi waliyoyabaini ikiwemo uchaguzi wa tuzo kutokuwa mzuri hali iliyopelekea  kuongezeka ushindani.

“Haijulikani kama ni uelewa mdogo au  kukosa umakini wa suala husika, vijana wengine waligombea tuzo ambazo hazikuwa ni stahiki yao wakiacha zile wanazostahili, pia uwezo wa kujieleza ulikuwa siyo mzuri kwani wengi waliweka maelezo mengi yasiyokuwa ya msingi wakati sisi tulikuwa tukihitaji vitu vichache ambavyo vitamfanya mtu aingie kwenye kinyang’anyiro,” amesema.

Tuzo hizo zimekuwa zikifanyika kwa mara ya tatu mfululizo sasa ambapo vijana wengi wamenufaika na kuweza kutoa fursa kwa vijana wengine.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...