Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza kulia)
akiangalia mitambo ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ya kurushia
matangazo iliyopo eneo la Kwemashai wilaya ya Lushoto mkoani Tanga
alipokuwa ziara ya kikazi ya siku mbili (Januari 7-8, 2020) kujionea
namna shirika hilo linavyoboresha usikivu wa matangazo yake ili
wananachi wa mkoa wa Tanga waendelee kupata haki yao ya Kikatiba ya
kupata taarifa kupitia shirika hilo. Wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya
Lushoto Januari Lugangika.

Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akisalimiana
na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela (kushoto) mara baada ya
kuwasili mkoani humo kwa ziara ya siku mbili (Januari 7-8, 2020)
kujionea namna Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) linavyoboresha
usikivu wa matangazo yake ili wananachi wa mkoa wa Tanga waendelee
wapate haki yao ya msingi ya kupata taarifa kupitia shirika hilo.

Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza kulia)
akiongea na wadau wa habari mkoani Tanga (hawapo pichani) wakati wa
ziara ya siku mbili (Januari 7-8, 2020) kujionea namna Shirika la
Utangazaji la Taifa (TBC) linavyoboresha usikivu wa matangazo yake ili
wananachi wa mkoa wa Tanga waendelee wapate haki yao ya msingi ya kupata
taarifa kwa kupitia shirika hilo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga
Martine Shigela.

Mhandisi wa Ufundi
Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Upendo Mbelle (wa pili kushoto)
akimsikiliza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe alipotembelea eneo Kwemashai wilaya ya Lushoto mkoani Tanga
iliposimikwa mitambo ya kurushia matangaz ya shirika hilo.

Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe
akisalimiana na baadhi ya viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya
wilaya ya Lusho mkoani Tanga.(Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Tanga)
………………
Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Tanga
Serikali
inaendelea kuboresha usikivu wa matangazo ya Shirika la Utangazaji la
Taifa (TBC) kwa kuimarisha mitambo ya kurushia matangazo katika maeneo
mbalimbali nchini ikiwemo kituo cha Mnyusi kilichopo Hale wilaya ya
Korogwe na Kwemashai wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa
kauli hiyo kwa nyakati tofauti katika wilaya za Korogwe, Lushoto pamoja
na Halmashauri ya jiji la Tanga alipokuwa ziaraya kikazi kwa siku mbili
mkoani humo kuanzia Januari 7-8, 2020.
Awali
katika kikao na wadau wa habari jijini Tanga, Dkt. Mwakyembe alisema
kuwa usikivu wa TBC Taifa mwaka 2015 ulikuwa ni asilimia 54 ambapo kwa
sasa baada ya hatua mbalimbnali kuchukuliwa na serikali usikivu umefikia
kiwango cha asilimia 73 na inatarajiwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2020
utafikia zaidi ya asilimia 90 nchi nzima.
“Lengo
la ziara yangu ni kukagua na kujionea utekelezaji na uboreshaji wa
usikivu wa urushaji wa matangazo ya TBC ili kuhakikisha wananchi
wanapata haki yao ya msingi ya Kikatiba ya kupata taarifa sahihi na kwa
wakati” alisema Dkt. Mwakyembe.
Kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara 18 (2) inabainisha kuwa
“Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio
mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na
shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.”
Katika
kutekeleza jukumu hilo Waziri Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Tanzania
imefanya vizuri kwa kuhama kurusha matangazo ya Televisheni (TV) kutoka
mfumo wa analojia na kuhamia mfumo wa kidijiti na kuifanya kuwa nchi ya
kwanza Afrika hatua ambayo imesaidia wananachi kupata taarifa ya habari
kupitia TV za ndani ya nchi bila gharama yeyote kupitia visimbuzi vyao.
Aidha,
Dkt. Mwakyembe amesema kuwa TBC ifanikiwa kupanua usikivu katika maeneo
mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo vitano katika wilaya za mpakani za
Rombo, Tarime, Kibondo, Kakonko, Namanga, Nyasa hadi Mbambabay
umekamilika. Wilaya za Ruangwa, Lushoto na Mtwara ambazo usikivu wake
ulikua hafifu umeimarika na mkakati wa Serikali ni kujenga mitambo ya
Redio katika mikoa ya Katavi, Njombe, Simiyu, Songwe, Unguja na Pemba.
Akimkaribisha
Waziri Dkt. Mwakembe, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela alisema
kuwa amefarijika kwa ziara hiyo mkoani humo kwani Waziri huyo amekuwa
kiongozi wa kwanza kutembelea mkoa huo kwa mwaka 2020 na ziara ina
manufaa kwa wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
“Mhe.
Waziri, ziara yako kwetu ni muhimu sana itasaidia wananchi kuhabarishwa
kwa kazi nzuri inayosimamiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na wewe unaendelea kuweka mazingira
mazuri ya wananchi kupata habari kwa usahihi na kwa wakati” alisema Mkuu
huyo wa Mkoa.
Waziri
Mwakyembe akiwa wilayani Lushoto, Mkuu wa wilaya hiyo Januari Lugangika
amesema kuwa wilaya yake inabaadhi ya maeneo ambayo bado yana
changamoto ya usikivu wa TBC yakiwemo Bumbuli, Mlalo pamoja na Umba,
hali inayowanyima wananchi kupata haki yao ya msingi ya kupata habari
kupitia chombo cha habari cha taifa.
Akitoa
taarifa kwa viongozi hao kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
TBC, Mhandisi wa Ufundi Upendo Mbelle amesema kuwa shirika hilo
linaendelea kuboresha usikivu wa TBC kwa kuweka mitambo midogo katika
maeneo yenye usikivu hafifu ili kufikia maeneo ya mabondeni na sehemu
zilizofichika nyuma ya milima.
Ziara
ya kikazi ya Dkt. Mwakeyembe inahusisha mikoa ya kanda ya kaskazini
katika katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na itahitimishwa mkoani
Arusha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...