Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii

RAIS Dkt.John Magufuli ametoa wiki moja kwa Waziri wa Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kuhakikisha anarudisha umiliki wa heka 750 kwa manispaa ya Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Februari 10 mwaka 2020 wakati akizindua majengo ya ofisi za Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam , Rais Magufuli amesema alishafuta hati ya eneo lenye ukubwa wa heka 750 ili zirudi Serikali na kisha kukabidhiwa kwa manispaa Kigamboni lakini kwa taarifa alizonazo hadi sasa bado umiliki upo Wizara ya Ardhi.

"Katika eneo hilo ambalo Mheshimiwa Mbunge (Mbunge wa Kigamboni Dk.Faustine Ndugulile)umezungumza , nilifuta hati ili liwe chini ya umiliki wa Serikali, lakini nimeambiwa bado liko chini ya umiliki wa Wizara ya Ardhi, bado haujarudishwa kwenye umiliki wa Manispaa ya Kigamboni. Najua mawaziri mko hapa, kamuelezeni Waziri mwenzenu wa ardhi ndani ya wiki mmoja umiliki uwe umesharudi manispaa.

"Umiliki wa ardhi hii uwe ndani ya Manispaa ya Kigamboni, ili wananchi wa Kigamboni wapange wanavyotaka na nitoe mwito kwa viongozi wa Kigamboni , ukubwa wa eneo hili ni heka 750, msije mkagawana na hapo ndipo mtakapojua kama mpo Kigamboni, Kisarawe au Mkuranga, lazima ardhi hii itunzwe na sio kwa ajili ya viongozi bali ni kwa ajili ya wananchi," amesema Rais Magufuli.

Amesisitiza kuwa eneo hilo ni kubwa na wananchi wanayo nafasi ya kuamua nini ambacho wanatakiwa kukifanya kwa ajili ya maendeleo yao, hivyo hatarajii kuona viongozi wa Kigamboni wanagawana eneo hilo.

Kuhusu kuzindua kwa majengo ya ofisi ya wilaya ya Kigamboni, Rais Magufuli amesema leo ni siku muhimu kwake kwa kushiriki kwenye uzinduzi wa majengo ya ofisi za Wilaya ya Kigamboni na kwamba wilaya hiyo inakuwa kwa kasi kwani idadi ya watu iliyopo ni 350,000.

Pia amesema Wilaya ya Kigamboni ndio kingo ya mboni ya macho ya Dar es Salaa na ndio kingo ya moyo wa Dar es Salaam na kuongeza kuwa idadi ya watu katika Jiji hilo imefikia milioni tano na inakadiriwa ikifika mwaka 2030 idadi ya watu itakuwa milioni 10.

"Mwaka 2016, Serikali ilianzisha Wilaya sita za Kigamboni, Ubungo, Kibiti, Marinyi, Songwe na Tanganyika na lengo ni kusogeza huduma karibu na wananchi.Nimefarijika leo kuzindua majengo ya ofisi ya wilaya ya Kigamboni, nawapongeza wote ambao wamehusika kukamilisha miradi hii ya ujenzi kama ilivyokusudiwa,"amesema.

Amesema kukamilika kwa majengo ya ofisi ya wilaya yataongeza hamasa ya watumishi kufanya kazi na matarajio yake wilaya hiyo itakwenda mbele kimaendeleo kwa kasi kubwa."Katika ujenzi wa majengo ya ofisi ya Wilaya ya Kigamboni nimeelezwa kuwa na Hospitali ya wilaya ya Kigamboni nayo iko hatua za mwisho kukamilika, pia vituo viwili vya afya navyo vimekamilika.

"Katika Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni nataka wakati inaendelea kumaliziwa ujenzi wake nataka dawa, madaktari na vifaa tiba vyote viwepo ili wananchi wapate huduma za afya.Nitashangaa Dk.Ndugulile kama utashindwa kusimamia haya maelekezo wakati uko pale Wizara ya afya.Hakikisheni dawa na madaktari wanakuwepo,Serikali imetumia Sh.bilioni 1.5 kujenga hii hospitali hivyo lazima ifanye kazi "amesema Rais Magufuli.
 RAIS Dkt.John Magufuli

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...