Na Janeth Raphael, Michuzi TV

HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam imezindua kituo cha huduma jumuishi za kitabibu, Polisi, Ustawi wa kijamii na kisheria kwa malengo ya kuwasaidia wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia huku ikielezwa asilimia 44 ya wanawake wamepitia ukatili wa kimwili katika maisha yao.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam baada ya kupokea kituo hicho jumuishi cha mkono kwa mkono katika hospitali hiyo Mwenyekiti wa bodi ya ushauri wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala Anna Maembe amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni jambo jema kwa kuwa masuala ya ukatili wa kijinsia ni changamoto inayoikabili jamii kwa kiasi kikubwa.

"Serikali yetu imeamua kulishughulikia tatizo hilo kwa nguvu zote ili kuhakikisha jamii unaishi kwa amani na wahanga wa ukatili huu wanapata huduma stahiki katika sehemu moja ambayo watakutana na watao huduma wote yaani polisi, waganga, ofisa Ustawi na wengine,"ameeleza.

Pia  Maembe ametoa shukrani za dhati kwa Jukwaa la utu na mtoto (CDF) kwa kujenga kituo hicho pamoja na Shirika linaloshughulikia masuala ya wakimbizi duniani (UNHCR) kwa kujenga vyoo na mabafu ambayo yatawasaidia sana wahanga wa ukatili wa kijinsia.

"Tunawashukuru sana CDF na UNHCR na tunaomba walengwa wote tukitumie kituo hiki na kujifunza vizuri," amesema.

Aidha amesema suala la ukatili wa kijinsia linagusa jamii nzima na ni wajibu wa kila mmoja katika kulisimamia na kuhakikisha linatokomezwa.

Kwa upande wake Mwakilishi mkazi wa UNHCR George Kuchio amesema kuwa mradi huo umegharimu Sh.milioni 40 huku akiipongeza hospitali hiyo kwa kuwa na kitengo hicho ambacho litawasaidia waathirika wengi wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Pia Kuchio amekipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili ambapo tafiti zinaonesha kuwa watoto 3 Kati ya 10 na mtoto wa kiume 1 kati ya saba wamekutana ukatili wa kingono kabla ya kutimiza miaka 18 na asilimia 75 ya wanaume na wanawake wamekutana na ukatili w kingono kutoka kwa watu muhimu wakiwemo ndugu na walimu.

Kituo hicho cha huduma jumuishi kitatoa huduma za haraka za vipimo, tiba, ushauri nasaha, Kinga ya VVU, kuchukua sampuli na kuhifadhia ushahidi, mazingira rafiki, faragha yanayozingatia utu na heshima kwa mhanga pamoja na kujenga imani kwa jamii na kuvunja ukimya.
 Mwenyekiti Bodi ya Ushauri Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala Anna Maembe na Mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa mataifa linashughulikia wakimbizi (UNHCR), Ndg.George Kuchio wakikata utepe kuashiria Ufunguzi wa Kituo cha Huduma Jumuishi.
 Mwenyekiti Bodi ya Ushauri Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala,Anna Maembe akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Huduma Jumuishi (Mkono Kwa Mkono)
Mwakilishi Kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi ,Ndg.George Kuchio akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo cha Huduma Jumuishi katika Hospitali ya Mwananyamala

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...