Kamishna wa Tume za Haki za Binadamu na Utawala Bora, Dkt. Fatma Rashid Khalfan akizungumza na wandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya wanawake mkoani Dodoma leo.
 Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Felista Bura akizungumza na wananchi mbalimbali waliojitokeza kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo kimkoa wa Dodoma yamefanyika jijini Dodoma.
 Watumishi wanawake kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakiwa kwenye maandamano ya siku ya wanawake duniani jijini Dodoma Leo.
 Watumishi wanawake kutoka Wizara ya Maji wakiwa kwenye maandamano katika siku ya wanawake duniani ambapo kimkoa wa Dodoma yamefanyika katika shule ya msingi Mkonze jijini Dodoma.
Wanawake mbalimbali waliojitokeza kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake mkoani Dodoma wakiwa kwenye maandamano ya pamoja.

Charles James, Globu ya Jamii
WANAWAKE nchini wametakiwa kutathimini mambo waliyoyafanya huku wakitajwa kupata mafanikio makubwa ikiwemo baadhi ya wanawake kwenye nafasi za maamuzi ndani ya serikali.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma katika siku ya wanawake duniani na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Dkt. Fatma Rashid Khalfan wakati akizungumza na wandishi wa habari.

Dkt. Fatma amesema kwa mara ya kwanza ndani ya historia ya Tanzania, Taifa limefanikiwa kuwa na Makamu wa Rais mwanamke ambaye ni Mama Samia Suluhu Hassan jambo ambalo linaonesha jinsi gani wanawake wamezidi kuaminiwa kwenye uongozi.

" Katika siku hii ya leo kikubwa zaidi tutambue kwamba Tanzania tumeridhia mkataba wa haki za binadamu hususani kwa wanawake na tukikumbuka kuna yale makubaliano ya wale wanawake wanaotoka Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 1995.

Hivyo kwa miaka hii 25 ya makubaliano ya mkutano ule ni wazi tunapaswa kujitafakari sisi kama wanawake na kutathimini ni hatua gani za kimaendeleo zimefanyika hasa katika jamii yetu na Taifa letu," Amesema Dk Fatma.

Amesema kwa awamu hii ya tano wanawake wamepiga hatua kubwa ya kuaminiwa ambapo kuna idadi kubwa ya Mawaziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu ambao wameteuliwa na Rais Dkt. John Magufuli jambo ambalo linaonesha kuwa uwezo wa wanawake siyo wa kutiliwa shaka.

" Kwa kweli namba ya viongozi wanawake kwa kipindi hiki imeongezeka, Tunavyozungumza leo Naibu Spika Dk Tulia Ackson ni mwanamke, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama ni mwanamke, Ummy Mwalimu ambaye ni Waziri wa Afya ni mwanamke. Hakiki nafasi yetu imeonekana," Amesema Dk Fatma.

Amesema wao kama Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora wataendelea kusimamia haki za wanawake pamoja na misingi ya utawala bora inazingatiwa.

Amesema katika mwaka huu wa uchaguzi wao kama Tume ya Haki wanawahamisha wanawake kujitokeza kuwania uongozi katika nafasi mbalimbali za kiuongozi.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma, Felista Bura amewataka wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi hasa katika nafasi za Ubunge na Udiwani huku akisema nafasi ya Rais imejaa.

" Huu ni mwaka wa uchaguzi niwaombe mjitokeze kuwania, ikifika Julai 1 madiwani na wabunge tunamaliza muda wetu njooni mgombee msiogope." Amesema Bura.

Maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani hufanyika Machi 8 ya kila mwaka ambapo mwaka huu kitaifa imefanyika Mkoani Simiyu ambapo mgeni rasmi alikua ni Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...