KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof.Elisante Ole Gabriel amewataka wafugaji nchini kuzingatia ubora wa mifugo yao na sio kuangalia zaidi wingi wa mifugo waliyonayo kwa kuwa ubora wa mifugo ndio utakaosaidia kupata mazao yaliyo bora yenye kuwanufaisha kiuchumi.
Alisema kuwa mfugaji akiweza kubadilika na kufuga kisayansi kwa maana ya kufuga kwa tija na akaanza kupata mazao ya mifugo yaliyo bora, ndipo hapo atakapofaidika na kazi yake ya ufugaji.
Katibu Mkuu ametoa wito huo leo (10.3.2020) wakati akiwakaribisha wawekezaji wa Kampuni ya kuchakata na kusambaza Nyama ya Tanfroz Limited inayomilikiwa na wawekezaji kutoka nchini Ubelgiji na Ufaransa, walipofika Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) jijini Dodoma kwa lengo la kutambulisha na kuomba ushirikiano katika mradi huo hapa nchini.
Prof.Gabriel aliongeza kuwa azma ya serikali hii ya awamu ya tano chini ya Rais, Dk.John Pombe Joseph Magufuli, inayosisitiza uchumi wa viwanda, haiwezi kufanikiwa vizuri bila kuboresha mifugo ambayo mazao yake hutegemewa kama malighafi za viwandani.
Katibu Mkuu aliwaahidi ushirikiano kutoka kwake na wataalam wake katika hatua mbalimbali kwa lengo la kufanikisha mradi huo ambao ukishaanza rasmi utawanufaisha wawekezaji na wafugaji wa hapa nchini na kwa majaribio alisema mradi huo umeanzia mkoani Iringa katika maeneo ya Mgagao ambapo kuna shamba lenye ng,ombe zaidi ya mia mbili.
Akiongea kwa niaba ya Kampuni hiyo, Mkurugenzi wa kampuni ya Tanftoz Limited Bw.Luc Battel, alisema kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya uwekezaji katika Sekta ya Mifugo kutokana na wingi wa mifugo iliyopo nchini, ila akasisitiza kuwa mifugo yenye manufaa ni ile yenye ubora unaotakiwa kitaifa na kimataifa.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa Tanzania itafanikiwa kupata zaidi masoko ya nyama katika nchi za mashariki ya mbali na kwingineko duniani iwapo tu ng,ombe au mbuzi watafugwa katika mazingira bora na kuepushwa na maradhi yakiwemo magonjwa ya miguu na midomo.
Aidha aliongeza kuwa uboreshaji wa mbari ni muhimu katika kupata mazao bora ya mifugo kwa maana ya nyama maziwa na ngozi ambayo hutumika kama malighafi katika viwanda mbalimbali hapa nchini.
Akiongea katika kikao hicho meneja wa kampuni ya CRV Bw.Hielke Sportel naye alisema kuwa ili kufanikiwa katika uboreshaji wa mbari nchini, ni vema wafugaji wakawa na ushirikiano katika kubadilishana mbari na elimu mbalimbali za ufugaji bora wenye tija.
Aidha taasisi ya utafiti wa mifugo nchini (TALIRI) na vyuo vya mafunzo ya mifugo pia zimetakiwa zitumike kuwainua wafugaji kwa kuwapelekea taarifa za tafiti na elimu mbalimbali za kuboresha mifugo yao kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti nchini (TALIRI) Dk.Eligy Shirima aliwashukuru wawekezaji hao kwa kutambua fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya mifugo na kuahidi kuwapa ushirikiano kila panapostahili ili kuwainua wafugaji nchini na hatimaye kuweza kutoa mchango katika uchumi wa taifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...