Rais wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Marais wa Afrika wanaopambana na Malaria (African Leaders Malaria Alliance (ALMA), ametangaza vipaumbele vyake vinne vitakavyokuwa msingi wa juhudi za kutokomeza malaria kote Afrika ifikapo mwaka 2030.

Vipaumbele hivyo vinavyotajwa kuleta mapinduzi makubwa, vinalenga kutafuta suluhu dhidi ya changamoto za mapambano ya kutokomeza malaria. Changamoto hizi zinajumuisha; ushiriki hafifu wa wanawake, watoto na vijana, uhaba wa fedha toka sekta za ndani, za umma na binafsi pamoja na tishio la kudumaa kwa michango ya wahisani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mheshimiwa Kenyatta alitangaza, “Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye vita hii ndani ya miaka kumi iliyopita, ili kuwa na Afrika Tunayoitaka kama ilivyoelezwa kwenye Mpango wa 2063, tusijisahau, badala yake tutafute na kupata raslimali zaidi zitakazotusaidia kutokomeza malaria na kuokoa maisha. Na ndiyo maana tumeainisha maeneo ya vipaumbele yatakayokuwa msingi wa utendajikazi wangu kama mwenyekiti wa ALMA:


1.       Matumizi ya dijitali na takwimu

Uanzishwaji wa majukwaa ya kidijitali yanayofika katika mataifa mbalimbali ili kusaidia upatikanaji na uwazi wa takwimu za mapambano dhidi ya malaria. Hii itasaidia kwa kiwango kikubwa juhudi zetu hasa katika maeneo yaliyoathirika zaidi. Mbinu hii itasaidia pia kuwa na tafiti za ndani ya Afrika hasa kwa kutumia taasisi za kitafiti zilizopo tayari ndani ya Afrika. Kwa kuimarisha upatikanaji wa takwimu, wananchi wote watakuwa na uelewa mzuri juu ya hatari zitokanazo na malaria na hivyo kuwawezesha kuchukua tahadhali mapema.

2.       Ushirikiano na Mashirika ya Kikanda ndani ya Afrika

Kwa kufanya kazi na mashirika ya kikanda ili kushirikiana na Wakuu wa Nchi na Serikali katika kujadili na kutatua changamoto kubwa na kutafuta majibu ya namna ya kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria. Hii itajumuisha matumizi ya teknolojia ili kuanzisha utaratibu wa kujitathimini na kufanya rejea kwa Wakuu wa Nchi na Serikali, kubadilishana uzoefu na kushauriana namna bora zaidi za kufuata, na kuanzisha tuzo kuwatambua wanaofanya vizuri zaidi katika ngazi ya kanda.

3.       Mabaraza na Mifuko ya kutokomeza Malaria

Kuanzisha walau Mabaraza mapya 15 ya kutokomeza malaria na kutafuta fedha zitakazosaidia kuongeza zaidi ushirikiano wa ngazi za juu wa sekta tofautitofauti ili kutia chachu juhudi za kupata fedha zaidi za ndani ikiwemo kutoka katika sekta binafsi.



4.       Makundi ya Ushauri ya Vijana

Kwa kushirikiana na viongozi vijana toka maeneo mbalimbali ya kiuongozi barani Afrika, kujenga “Jeshi la Vijana” dhidi ya malaria. Kikosi-kazi hiki cha mabalozi vijana kitaanzisha ushirikiano wa kisiasa, utafutaji wa fedha, ubunifu, utafiti na maendeleo na hata kuundwa kwa kada ya watu wanaopambana dhidi ya malaria.

“Vipaumbele vya Mheshimiwa Rais Kenyatta tayari vimepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika. Tunatambua kwamba kufanikiwa kwa vipaumbele hivi vinne kutachochea zaidi mapambano ya kuhakikisha Bara letu la Afrika linatokomeza kabisa ugonjwa huu,” alisema Kamishina wa Masuala ya Jamii wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mheshimiwa Amira El-Fadil.

Dr. Abdourahmane Diallo, ambaye ni Mtendaji Mkuu wa ushirikiano wa RBM wa Kutokomeza Malaria, alisema, “Uongozi toka kwa viongozi wa nchi na serikali Barani Afrika ambao kutokomeza malaria ni moja ya sera zao muhimu za kisiasa, ni muhimu sana katika vita hii. Ninaamini kwamba vipaumbele vinne vya Rais Kenyatta, vikiongozwa na ubunifu na ushirikishwaji wa wadau wote ndio njia sahihi ya kufikia malengo ya kutokomeza malaria. Vitahakikisha pia kwamba kuna raslimali mpya na jamii mpya zimejumuishwa kwenye vuguvugu hili la kutokomeza kabisa malaria.”

Ugonjwa wa malaria unabaki kuwa changamoto kubwa inayolikabili bara la Afrika. Kiasi cha 93% ya wagonjwa wote wa malaria duniani wanapatikana Afrika huku 94% ya vifo vyote ulimwenguni vinavyotokana na malaria navyo vikitajwa kutokea barani humo. Kuna haja ya kuchukua hatua za haraka hasa katika mataifa 10 yaliyoko ndani ya Umoja wa Afrika ambayo yanachangia 67% ya wagonjwa na 62% ya vifo ulimwenguni kote. Mataifa hayo ni Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Cote d’Ivoire, Msumbiji, Niger, Burkina Faso, Mali, Angola na Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...