WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano iko imara na inamipango madhubuti ya kuwahudumia na kuwatumikia Watanzania katika maeneo yote nchini.

Ili kutimiza adhima hiyo, Waziri Mkuu amepiga marufuku kitendo cha watumishi wa umma kumaliza wiki wakiwa maofisini na badala yake amewataka watumie siku nne kwenda kwa wananchi katika maeneo yao.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni  (Jumatatu, Machi 2, 2020) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM Maramba wilayani ya Mkinga, Tanga.

“Ni lazima wananchi wahudumiwe wakati wote. Watumishi wa umma ni marufuku kumaliza wiki nzima mkiwa ofisi mnatakiwa kutumia siku mbili ofisini na siku nne zilizobaki nendeni mkasikilize kero za wananchi katika maeneo yao na kuzipatia ufumbuzi,”

Pia, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wahakikishe fedha zote zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinatumika kama ilivyokusudiwa. “Fedha hizi tunazoleta ni za moto zisidokolewe zitawaunguza.”

Kufuatia changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya ya Mkinga, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo watenge fedha za mapato ya ndani na kuanzisha miradi ya uchimbaji wa visima wakati Serikali ikiendelea kulishughulikia suala hilo.

Kadhalika, Waziri Mkuu alimuagiza Mganga Mkuu wa wilaya ya Mkinga ahakikishe wananchi wanaokwenda kufuata huduma za matibabu katika vituo vya afya na zahanati wanapatiwa dawa badala ya kuelekezwa kwenda kununua kwenye maduka.

Alisema Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka sh. bilioni 37 hadi sh bilioni 269, hivyo hakuna sababu ya mwananchi kwenda kwenda eneo la kutolea huduma ya afya na kukosa dawa. “Lazima mhakikishe dawa zote zinazotakiwa zinakuwepo kwenye zahanati  na hivyo hivyo kwenye vituo vya afya na hospitali.”

Kuhusu ombi la mbunge wa Mkinga Danstan Kitandula la kutaka wananchi wapewe mashamba yasiyoendelezwa ili waweze kuyatumia katika shughuli za kilimo, Waziri Mkuu alisema atalifanyia kazi suala hilo.

Pia, Waziri Mkuu aliwataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao na kwamba changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za upatikanaji wa huduma za maji, umeme na miundombinu ya barabara zitafanyiwa kazi.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo na wilaya ya Mkinga ili kuwawezesha wananchi hasa wanawake kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kutumia muda wao mwingi kutafuta maji.

Waziri Mkuu alisemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.

Kuhusu suala la upatikanaji wa umeme, Waziri Mkuu alisemamaeneo hayo yatasambaziwa umeme kupitia Mradi wa Nishati Vijijini (REA) na wananchi hawatowajibika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

“Rais wetu Dkt. John Magufuli anataka kuona nyumba ya kila Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo na vya wilaya hii ya Mkinga. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”

Kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alizindua miundombinu ya kituo cha afya cha Maramba ambayo ilifanyiwa ukarabati na kusema kwamba Serikali itaendelea kukiimarisha kituo hicho ili kukiboresha huduma za afya kwa wananchi.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mganga wa Kituo cha Afya cha Maramba wilayani Mkinga, Dkt. Kidai Nyaleja wakati alipotembelea  chumba cha upasuaji katika kituo hicho, Machi 2, 2020.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Veronica Msaki ambae amejifungu mtoto wa kike Doreene (pichani) katika Kituo cha Afya cha Maramba wilayani Mkinga. Mheshimiwa Majaliwa alitembela   wodi ya wazazi katika kituo hicho, Machi 2, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Madaktari na Wauguzi wa Kituo cha Afya cha Maramba wilayani Mkinga baada ya kutembelea kituo hicho, Machi 2, 2020. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa wa kambi ya Maramba wakati alipowasili kwenye uwanja wa CCM Maramba kuhutubia mkutano wa hadhara, Machi 2, 2020.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisikiliza kwaya ya Jeshi la Kujenga Taifa, Kambi ya Maramba wilyani Mkinga wakati alipowasili kwenye uwanja wa CCM Maramba kuhutubia mkutano wa hadhara , Machi 2, 2020. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela.
 Vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa wa Kambi ya Maramba wakiimba katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika uwanja wa CCM  Maramba, Machi 2, 2020.
 Baadhi ya wananchi wa Maramba  wilayani Mkinga wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa CCM Maramba akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga, Machi 2, 2020.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa CCM Maramba wilayani Mkinga, Machi 2, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...