KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imetoa ushauri  kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuongeza  uwekezaji  katika  kuendeleza  Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini baada ya kuridhishwa na utendaji wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela katika eneo hilo.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe Peter Serukamba wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo  jijini Arusha.

Mhe Serukamba amesema Chuo cha Nelson Mandela kinafanya vizuri kwenye matumizi ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu na kuwa inaridhisha kuona kuna vifaa vya Tehama vinavyoendana na Mapinduzi ya nne ya Viwanda ikiwemo kompyuta kubwa yenye uwezo wa kuchakata taarifa mbalimbali kwa muda mfupi "High Performance Computting sysytem (HPC) au "Super Computer" ikilinganishwa na kompyuta za kawaida yenye gharama ya takribani Dola za kiamarekani milioni 1.3.

"Nimeridhishwa  na maendeleo ya kazi za utafiti na ubunifu  katika Taasisi hii hasa jinsi mlivyoweza kuingia katika Mapinduzi ya nne ya viwanda, rai yangu kwa Serikali ni uwekezaji zaidi katika eneo hili ili tafiti na ubunifu unaozalishwa  uwe na manufaa zaidi kwa wananchi " Amesisitiza Mhe Serukamba.

Kwa upande wake mjumbe wa Kamati hiyo ambae pia ni mbunge wa Biharamulo Magharibi Oscar Mukasa amesema  ni vizuri kukaanzishwa chombo katika Chuo hicho  ambacho kitasaidia kuhusianisha ufanisi wa tafiti zinazozalishwa na utekelezaji wa Sera.

Nae Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Tano imetoa kipaumbele katika eneo la Sayansi na Teknolojia kwani ni ndicho kichocheo kikubwa cha uimarishaji Viwanda.  

Katika hatua  nyingine Prof. Ndalichako amesema Wizara anayoisimamia  itatoa fedha kiasi cha sh bilioni 3.9 kwa ajili ya ujenzi wa Hosteli za wanafunzi wa kike katika Chuo hicho ili kuongeza idadi ya wanafunzi  wanawake wanasayansi na watafiti nchini.

Kwa upande wake  Makamu Mkuu wa  Chuo hicho Prof. Emmanuel Luoga amesema Chuo kimefarijika sana na ujio wa Kamati na kwamba  kitaendelea kujikita katika dhamira yake ya kufanya tafiti katika Sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na kupeleka matokeo  kwa walaji.
 Wziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako  pamoja na wabunge wanawake ambao ni wajumbe  wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakiwa kwenye picha ya pamoja na mtafiti mwanamke (aliyevalia gauni jekundu) baada ya kuelezea tafiti yake aliyofanya na kupata dawa ya kulainisha ngozi wakati walipotembelea Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
 Wziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako  pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakipata maelezo juu ya mfumo  kusafisha maji uliotengenezwa na  Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela wakati walipotembelea Taasisi hiyo.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba (aliyekaa katikati)akiwa kwenye picha ya pamoja na Mawaziri wanaosimamia Elimu, wajumbe wa Kamati anayoisimamia,  Menejinenti na Watumishi wa Taasisi ya Nelson Mandela wakati walipotembelea Taasisi hiyo kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba (wa tatu kutoka kulia) na Makamu Mwenyekiti Juma Nkamia (wa tatu kulia) wakiongozana na Mawaziri wanaosimamia Elimu wakati walipowasili katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Jijini Arusha kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa katika Taasisi hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...