Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde akihutubia
watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu)
wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika
Machi 8, 2020 Jijini Arusha.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la
Wafanayakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu) wakisikiliza hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (hayupo
pichani).
Katibu wa Baraza la Wafanyakazi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew
Massawe akieleza jambo wakati wa mkutano huo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (katikati
waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la
Wafanayakazi wa Ofisi hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (katikati
waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Idara na Wakuu
wa Vitengo wa Ofisi hiyo mara baada ya mkutano huo wa Baraza la
Wafanyakazi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde akiimba
wimbo wa Shikamano “Solidarity” pamoja na Wajumbe wa Baraza la
Wafanyakazi wa Ofisi hiyo pamoja na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi hiyo
WCF, OSHA, PSSSF, NSSF na CMA.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
……………………………………………………………………………………………….
Na: Mwandishi Wetu
Wajumbe wa Baraza
la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu wamehimizwa kutekeleza majukumu kwa ufanisi na weledi ili
kuimarisha utendaji kazi wao.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony
Mavunde ametoa kauli hiyo hii leo Jijini Arusha alipokuwa akifungua
Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo uliyofanyika katika
ukumbi wa Mkutano uliyopo katika hoteli ya Gold Crest, Machi 8, 2020.
Alieleza kuwa
uwepo wa Baraza la Wafanyakazi katika sehemu za kazi unasaidia kuongeza
ushirikishwaji wa watumishi katika kupanga na kutekeleza majukumu yao,
kuleta usawa katika kujadili mambo muhimu, kutoa ushauri juu ya tija na
ufanisi wa kazi ikiwemo kukumbushana, kuelimishana na kuweka mazingira
bora ya utendaji kazi na kuweka umoja kati ya wafanyakazi na viongozi.
“Ni matumaini
yangu Baraza hili litakuwa na mijadala yenye uwazi na mambo
yote yatakayojadiliwa yatasaidia kuimarisha utendaji wa majukumu ya
Ofisi kwa lengo la kuhakikisha mazingira ya utendaji kazi yanaboreshwa
kwa manufaa ya kutoa huduma bora kwa wananchi, inajulikana kuwa Ofisi ya
Waziri Mkuu ina mambo mengi yanayogusa jamii moja kwa moja na hasa
masuala ya Kazi, Ajira, maendeleo ya vijana na watu wenye ulemavu,”
alisema Mavunde.
Aliongeza kuwa ni
muhimu kwa kila mjumbe wa Baraza hilo kutumia nafasi aliyopewa ili
uwakilishi wake uweze kuleta tija na kuwa chachu katika kuleta maendeleo
ya watumishi wote kwa ujumla.
Sambamba na hayo
Naibu Waziri Mavunde alitoa maagizo kwa Wajumbe wa Baraza ikiwemo suala
la kusimamiwa vizuri sekta ya kazi hususani kuongezwa jitihada za zaidi
katika kufanya kaguzi mara kwa mara ili kuhakikisha sheria na kanuni za
kazi hapa nchini zinafuatwa.
Pia alitilia
mkazo juu ya matumizi ya teknolojia katika kuwahudumia wananchi kwa
haraka na wepesi, hivyo alihimiza Baraza hilo kuandaa mpango endelevu
utakao wawezesha watumishi kujifunza matumizi ya teknolojia mpya ambayo
ni dhabiti katika kutoa huduma.
Aidha, Mheshimiwa
Mavunde alitoa wito kwa kila mjumbe wa baraza hilo kushirikiana na
watumishi wenzao na wote kwa pamoja watambue kuwa wanao wajibu wa
kufanikisha malengo ya Serikali na Ofisi hiyo.
Halikadhalika
aliwasihi wajumbe wa baraza hilo kuendelea kutekeleza taratibu na sheria
za kupambana na masuala ya rushwa katika maeneo ya kazi. Pamoja na hayo
alipongeza utendaji wa watumishi wa ofisi yake kwa utekeleza wa
majukumu mbalimbali ikiwemo ubunifu katika kuratibu programu ya Taifa ya
Kukuza Ujuzi, kwa lengo la kulinda mazingira ya kazi na ajira nchini,
kuanzishwa kwa mfumo wa kielektroniki wa vibali na uratibu wa mfuko
mfuko wa maendeleo ya Vijana ambao unawezesha vijana kiuchumi.
Awali wakati
wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Baraza hilo la Wafanyakazi alisema kuwa majadiliano ambayo
yamekuwa yakifanyika katika mkutano wa baraza hilo yamekuwa
yakisaidia kutatua changamoto zinazojitokeza sehemu ya kazi na pia
kuboresha mazingira ya utendaji na kazi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...