WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) Selemani Jafo amelitaka Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) na Taasisi ya Elimu Tanzania(TET), kuhakikisha utaratibu wa kufanya marejeo ya mitihani ulioanza kwa kidato cha sita uhusishe madarasa yote yanayotarajia kufanya mitihani ya Taifa.

Aidha, amewataka wanafunzi kuzingatia ratiba ya masomo inayotolewa ili wasikose vipindi vinavyorushwa kwenye redio,runinga na mitandao ya kijamii.

Jafo ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utaratibu wa masomo kwa njia ya runinga,redio na mitandao ya kijamii.

Amezitaka taasisi hizo kuangalia utaratibu huo wa marejeo kwa madarsa mengine kama kidato cha pili,cha nne,darasa la saba na la nne ili nao wawe na umahiri katika kujibu mitihani yao.

Amesema Serikali kupitia wadau mbalimbali imetoa fursa hiyo muhimu ambayo inapaswa kuzingatiwa na watu wote wakiwemo wazazi,walimu na wanafunzi wenyewe.

“Niwatake wanafunzi wote hasa wa kidato cha sita ambao sasa maandalizi ya kufanya marejeo yanafanyika, tutumie fursa hii vizuri ya kujiandaa kwa utaratibu mpya utakaotumika kuanzia mwaka huu wa kupima umahiri tofauti na ule wa awali wa kuulizana maswali tuliouzoea,”alisema Jafo.

Ameongeza kuwa “Wanafunzi tumieni fursa hii iliyoletwa kwenu,zingatia ratiba,jipimeni uwezo wenu  ili wenzio wasikuache nyuma pindi mkirudi shuleni,someni kwa bidii kwa  maana tunataka kuelekea kwenye Taifa lenye uchumi imara.”

Amewataka walimu kutumia fursa hiyo kujijengea uwezo wao wenyewe pia lakini kuwawezesha kuwa na uelewa zaidi ili wanafunzi wao watakapohitaji msaada pale watakapokwama wawe wanajua nini kinachoendelea.

“Walimu wetu najua mtu huwezi kuwa mkamilifu kwenye maeneo yote,kwa upande wenu hii pia ni fursa ya kujijengea uwezo kupitia walimu waliopo kwenye program hii ili ukirudi shuleni unakuwa umeongeza kitu kipya,lakini mwanafunzi wako anaweza kukupigia simu ameshindwa kuelewa sehemu Fulani hivyo inakuwa rahisi kumuelewesha,” Amesema Jafo.

Waziri Jafo amesema kama Waziri anayesimamia elimu ya awali,msingi na sekondari amefarijika kuanza kwa utaratibu huo na ni imani yake kuwa pengo la vijana waliokuwa wanakaa nyumba bila ya msaada wowote wa kimasomo linaenda kuzibika.

“Wazazi wapeni nafasi watoto wenu ya kushiriki vipindi vyote vinavyotolewa, inawezekana vipindi vinaendelea wewe mzazi umempa mtoto wako kazi nyingine anafanya hilo sio sahihi, toa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha watoto wanasoma na kufanya mazoezi yote yanayotolewa na walimu,”Amesisitiza Jafo.

Jafo amevitaja vyombo vya habari ambavyo vinashiriki katika mpango huu wa ufundishaji wa vipindi kwa njia ya Televisheni na Radio kuwa ni TBC, ZBC, Azam Tv, Channel Ten, Clouds Fm, Global Tv, Gel Tv na Radio mbalimbali.

Pia aliwakumbusha wazazi na wanafunzi wote kuwa vipindi hivyo vitakua vinarushwa kupitia mtandao wa Youtube kwa ajili ya marudio ili kujenga uelewa zaidi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...