Na Jonas Kamaleki- MAELEZO, Tarime

Kahawa ni moja ya mazao ya kimkakati zao ambalo limebadili maisha ya wakazi wa Tarime, Mkoa wa Mara kwa kuwaongezea kipato hivyo kuwaletea maendeleo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tarime, Apoo Castro Tindwa akizungumza na maafisa wa Idara ya Habari (MAELEZO) katika mahojiano maalum amesema juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kufufua zao la kahawa zimewanufaisha wananchi wa Tarime.

“Zao la kahawa limeibuka upya kupitia Serikali ya Awamu ya Tano na kahawa ya Tarime imeonekana kuwa kahawa bora Afrika, jambo ambalo sisi wakazi wa maeneo haya tunajivunia sana”, alisema Tindwa.

Juhudi za kukuza kilimo hasa cha kahawa Tarime ni pamoja na kuandaa wataalam wakubwa na wadogo, kutenga fedha zaidi ya Tsh. milioni 55 kwa ajili ya kilimo, kutafuta masoko na kujenga kiwanda cha kubangua kahawa.

Wilaya ya Tarime imejiwekea lengo la kuzalisha kahawa hadi kufikia tani 5000 kwa mwaka.

Naye mkulima mkufunzi wa kahawa, Petro Mwita Burungo anayefahamika kwa jina la Nyeusi amesema kuwa kahawa inayolimwa kisasa imemuongezea kipato ambacho kimemuwezesha kusomesha watoto shule, kujenga nyumba ya kisasa ya kuishi na kupata fedha ya kuweka akiba benki.

Kwa mujibu wa Bw. Mwita ukulima wa kisasa kwa mche mmoja anapata kilo 5 za kahawa ambapo zamani kwa kilimo cha mazoea alikuwa akipata kilo 2 tu za kahawa kwa mche, hivyo maisha yake yamebadilika na maendeleo ni dhahiri.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufufua vyama vya ushirika, AMCOS ambavyo vinanunua kahawa na kutulipa kwa wakati”, anasema Mwita.

Mwita ameendelea kusema kuwa Serikali imemuinua mkulima wa chini na kumpandisha juu kuliko ilivyokuwa kwa vipindi vilivyopita ambapo baadhi ya wananchi walianza kung’oa mibuni na kupanda mazao mengine kwani zao hilo lilionekana kukuso tija.

Mkulima huyu anazalisha mbegu za kisasa za kahawa kwa njia ya vikonyo ambavyo vikishapandwa vinatoa mazo mengi na hukomaa kwa muda mfupi ikilinganishwa na mbegu za kizamani.

Kwa upande wake Mkazi wa Kijiji cha Nyarero, Wilaya ya Tarime, Joyce Mwita amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imewajali sana wakulima wadogo na kuwainua kwa kuwaletea wataalaam wa kilimo ambao wamewapatia mafunzo ya kilimo bora cha kahawa.

“Kwa kweli namshukuru sana Rais John Pombe Magufuli kupitia wataalaam wake kufufua zao la kahawa, kwa sasa hata tunapozalisha miche tunapata wateja na tunapouuza kahawa tunapata fedha yetu pasipo usumbufu ikilinganishwa na zamani tulivyokuwa tukiumizwa na walanguzi”, anaongeza Joyce.

Mkulima mwingine wa kahawa aliyonesha kunufaika na zao hilo ni Bw. Boniface Gamo ambaye licha ya kulima anazalisha miche ya kahawa. Anasema kuwa zao hilo limemuongezea kipato kwa kiwango kikubwa na hivyo kumuweza kusomesha watoto na kufanya maendeleo mengine.

“Tunazalisha miche ambayo tunaiuza kwa wakulima na kujipatia fedha nyingi, kwa sasa tumezalisha zaidi ya miche 350,000 na kuisambaza kwawananchi, hakika Serikali ya rais magufuli imetujali sisi wakulima”, ameongezea Gamo.

Zao la kahawa ni kati ya mazao yanayoliingizia Taifa fedha za kigeni kwa maana soko lake liko ndani na nje ya nchi.

Serikali ya Awamu ya Tano imefufua zao hilo kwa kuanzisha taasisi za utafiti wa kilimo kwa ajili ya kulipa nguvu zao la kahawa.

Mfano Taasisi ya Utafiti wa kahawa nchini (TACRI) - Maruku inafanya utafiti wa kahawa na kuzalisha mbegu bora, inaotoa mafunzo kwa wakulima kuhusu mbegu bora, kilimo cha kutumia mbolea na kupambana na magonjwa ya zao la kahawa.

Wakulima wanopata mafunzo ya utafiti wa kahawa na kuzingatia kanuni bora za kilimo, maisha yao kiuchumi yamebadilika na wanapongeza juhudi za makusudi za Serikali za kufufua na kutilia mkazo zao hilo muhimu katika uchumi wa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.

Hapa Tanzania kahawa inalimwa kwa wingi katika mikoa ya Kagera, Kilimanjaro, Mara na Ruvuma. Zao hili ni la kibiashara katika mikoa tajwa na maeneo mengine ya nchi ambalo linawanufaisha wananchi kiuchumi. 
Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...