Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza na kuwatakia
heri Wafanyakazi wote hapa nchini ambao leo tarehe 01 Mei, 2020 wanaadhimisha
siku ya wafanyakazi (Mei
Mosi).
Mwaka huu sherehe
za Mei Mosi hazitafanyika ili kuepusha mikusanyiko ya watu, ikiwa ni hatua
muhimu ya kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa
na virusi vya Corona (Covid-19).
Mhe. Rais Magufuli
amesema licha ya kwamba sherehe za Mei Mosi hazitafanyika mwaka huu, Serikali
inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Wafanyakazi katika ujenzi wa Taifa na
itaendelea kusimamia maslahi yao na kuboresha mazingira ya kazi.
Amewataka
Wafanyakazi hao kuendelea kuchapakazi kwa juhudi na maarifa ili Watanzania
waendelee kunufaika na huduma wanazozitoa katika maeneo yao ya kazi huku
wakichukua tahadhari zote zinazoelekezwa na wataalamu juu ya kujikinga na
ugonjwa wa Corona.
“Ndugu Wafanyakazi wenzangu
nawapongeza sana kwa kuchapa kazi, mimi nipo pamoja nanyi na natambua kazi
nzuri mnayoifanya, nawaomba katika kipindi hiki ambacho dunia inapita katika
wakati mgumu wa kukabiliana na ugonjwa wa Corona, sisi tuendelee kuchapakazi,
kamwe ugonjwa huu usiwe sababu ya kurudi nyuma na kuacha kuwahudumia
Watanzania, mimi naamini Mwenyezi Mungu atatuvusha”
amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
amewapongeza Waajiri wote wa Serikali na Sekta Binafsi, na ametoa wito kwao kutotumia
ugonjwa wa Corona kama kigezo cha kuwanyanyasa wafanyakazi.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
01 Mei,
2020
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...