Charles James, Michuzi TV

WANANCHI wametakiwa kuvitunza na kuvithamini vifaa vya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona vinavyotolewa na wadau mbalimbali nchini katika kusaidia kujikinga na ugonjwa huo.

Kauli hiyo imetolewa wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro na Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk Msuya, Dk Ombeni Msuya wakati akikabidhi mashine za kisasa za kunawia mikono kwenye Misikiti na Zahanati wilayani humo.

Taasisi hiyo ya Dk Msuya imekua ikiiunga mkono serikali katika sekta mbalimbali ikiwemo pia ya Elimu na toka ugonjwa wa Corona uingie nchini imekua ikihamasisha wananchi kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo kama ambavyo serikali imekua ikisisitiza.

Dk Msuya amesema mashine hizo zitasaidia wananchi kutumia maji na sabuni kwa kukanyaga kwa miguu bila kutumia mikono jambo ambalo linapunguza pia uwepo wa maambukizi kwenye koki za bomba kwa kila mtu kuigusa.

" Lengo la misaada yetu hii ambayo pia tumegawa kwenye Taasisi za Dini ya Kikristo, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na maeneo mengine ni kuiunga mkono serikali yetu ambayo chini ya Rais Magufuli imechukua hatua mbalimbali za kuwakinga wananchi na ugonjwa huu.

Hivyo niwaombe wote mtakaotumia vifaa hivi tuvitunze kwani hatujui Corona itaisha lini. Lakini pia tuvitumie ipasavyo ili tuweze kuepukana na maambukizi ya ugonjwa huu," Amesema Dk Msuya.

Amebainisha kuwa mashine zilizokabidhiwa kwenye Misikiti hiyo wilayani Mwanga ni 10 na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuwahudumia watanzania.

Kwa upande wake Katibu wa Bakwata Wilaya ya Mwanga, Ustaadhi Iddi Mchome ameishukuru Taasisi hiyo kwani vitakua msaada kwa Waislamu na wasio waislamu katika kujikinga na Corona.

Ustaadhi Mchome amesema walikua wanakabiliwa na changamoto ya kutumia vifaa duni ambavyo kila mtu atashika mkono wakati wa kunawa lakini kupitia mashine hizo sasa zitakua msaada kwani ili unawe inabidi utumie miguu kubonyeza mashine hizo.

" Kwa niaba ya waislamu wa Wilaya ya Mwanga tunaishukuru sana Taasisi hii, mmeonesha moyo wa kizalendo sana kwetu sisi. Hatuna cha kuwalipa zaidi ya kuwaombea dua na kuvitunza vifaa hivi," Amesema Ustaadhi Mchome.
 Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk Msuya, Dk Ombeni Msuya akikabidhi mashine za kunawia kwa Katibu wa Bakwata Wilaya ya Mwanga, Ustaadhi Iddi Mchome kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa Corona.
 Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk Msuya, Dk Ombeni Msuya (kushoto) akikabidhi mashine ya kunawia kwenye Zahanati ya Sungo wilayani Mwanga, Kilimanjaro kwa ajili ya kujikinga na Corona. Katikati ni Diwani wa Kata ya Msangeni iliyopo Zahanati hiyo, Fihiri Mvungi na kulia na Mganga Mfawidhi wa Zahanati hiyo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk Msuya, Dk Ombeni Msuya akikabidhi mashine za kunawia kwa ajili ya kujikinga na Corona kwa Ustaadhi wa Msikiti wa Msambeni wilayani Mwanga, Kilimanjaro Ally Swalwa (wa kwanza kulia).
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...