Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof Keneth Bengesi kukagua maghala ya kuhufadhia sukari Jijini Dar es salaam, leo tarehe 16 Mei 2020 wakati akifanya ziara ya kushtukiza Jijini Dar es salaam ili kukagua na kujionea hali ya upatikanaji wa sukari nchini. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof Keneth Bengesi wakishusha na kukagua sukari zilizopo kwenye makontena kwenye maghala ya kuhufadhia sukari Jijini Dar es salaam, leo tarehe 16 Mei 2020 wakati akifanya ziara ya kushtukiza Jijini Dar es salaam ili kukagua na kujionea hali ya upatikanaji wa sukari nchini.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisaini kitabu cha wageni  mara baada ya kutembelea Bodi ya sukari kabla ya ziara ya kukagua maghala ya kuhufadhia sukari Jijini Dar es salaam, leo tarehe 16 Mei 2020. Mwingine pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof Keneth Bengesi
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua maghala ya kuhufadhia sukari Jijini Dar es salaam, leo tarehe 16 Mei 2020 wakati akifanya ziara ya kushtukiza Jijini Dar es salaam ili kukagua na kujionea hali ya upatikanaji wa sukari nchini.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Serikali imetangaza kuendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria  wafanyabiashara nchini wanaotumia uwepo wa ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID 19) kuhodhi kiasi cha sukari kinachokuwa kwenye mzunguko na kuuza kwa bei ya juu zaidi ya bei ya ukomo katika eneo husika ambayo ni kati ya Shilingi 2600 hadi 3200.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 16 Mei 2020 wakati akifanya ziara ya kushtukiza Jijini Dar es salaam ili kukagua na kujionea hali ya upatikanaji wa sukari nchini.

Mhe Hasunga amesema kuwa serikali imeweka mbinu kali za kuwabaini wafanyabiashara hao na punde watakapobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ametangaza hali ya upatikanaji wa sukari nchini kuwa imeendelea kuimarika ambapo kufikia tarehe 16 Mei 2020 kiasi cha Tani 18,142 kimeingia nchini kati ya kiasi cha Tani 40,000 kilichoagizwa na wazalishaji wa ndani kwa ajili ya kuziba pengo la uzalishaji wa msimu wa mwaka 2019/2020.

Amesema kati ya kiasi hicho cha Tani 18,142 kilichoingizwa kiasi cha Tani 15,498 kimetolewa bandarini na mipakani na tayari kipo sokoni na kingine cha Tani 2,644 kipo katika hatua mbalimbali za kutolewa bandarini.

Amebainisha kuwa tarehe 16-22 Mei 2020 zitaingia Tani 7470, Tarehe 23-31 Mei 2020 zitaingia Tani 13,404, huku tarehe 1-4 Mei 2020 kiasi cha Tani 984 kitawasili nchini.

Kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali kukabiliana na upandaji holela wa bei, Waziri Hasunga amesema kuwa serikali ilitoa bei elekezi kupitia GN Na 284 na 352 ya tarehe 24 Aprili 2020 na tarehe 8 Mei 2020 mtawalia, na kufanya msako wa wafanyabiashara wasio waadilifu wanaouza sukari kinyume na bei elekezi kwa kushirikiana na mamlaka zingine za kiserikali.

Hatua nyingine ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wafanyabiashara waliobainika kuuza sukari kinyume na bei elekezi ambapo jumla ya wafanyabiashara 51 wamekamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Kadhalika, Waziri Hasunga amesema kuwa serikali ilifanya marekebisho ya GN kwenye mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Dodoma, Singida na Tabora.

Katika Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga bei ya sukari haitakiwi kuzidi Shilingi 2,800 kwa mlaji kwa kiasi cha kilo moja, Mkoa wa Singida, Tabora na Dodoma bei ya sukari haitakiwi kuzidi shilingi 2,900 kwa mlaji huku katika Mkoa wa Dar es salaam bei ikitakiwa kutozidi shilingi 2,600 kwa mlaji.

Mhe Hasunga amesema kuwa tatizo la upungufu wa sukari kutokana na sababu mbalimbali lilikwishapatiwa ufumbuzi hivyo wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi na jambo hilo huku akitolea mfano kampuni ya Alnaeem Enterprises ambayo imekuwa na sukari toka jumatano kiasi cha Tani 1,400 ambapo ina kiasi kikubwa cha sukari lakini mkoa wa Dar es salaam wamekuwa na malalamiko ya kukosekana kwa sukari.

Kwa kawaida msimu mpya wa sukari huanza mwishoni mwa mwezi Juni, Serikali kupitia Bodi ya Sukari tayari imefanya mazungumzo na kiwanda cha sukari cha Kilimbero ambapo wamekubali kuanza uzalishaji tarehe 21 Mei 2020 huku ikiendelea kufanya mazungumzo na wazalishaji wengine ili kuanza uzalishaji mapema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof Keneth Bengesi amesema kuwa Bodi hiyo itaendelea kufanya mawasiliano na Mamlaka ya Bandari ya Tanzania ili kuhakikisha kuwa sukari zote zinazoingia bandarini ziweze kutolewa kwa wakati ili iweze kusambazwa na kuwafikia watumiaji haraka iwezekenavyo.

Amesema kuwa kadri itakavyokuwa inafika bandarini itakuwa inatolewa kwa wakati huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kuiamini serikali kuwa serikali ipo makini katika utekelezaji wa majukumu yake hivyo wananchi wasiwe na mashaka yoyote kuhusu  sukari kwani inafanya kazi kutatua kadhia hiyo.

Katika kipindi cha miaka mitatu serikali imeweka mikakati ya kujitosheleza kwa sukari nchini ambapo kutakuwa na ongezeko la uzalishaji wa miwa na sukari nchini kupitia miradi ya Bagamoyo Sugar, Mkulazi II, S.J Sugar Mtwara, Morogoro Sugar, na shamba la Hekta 25,000 lililopo Kigoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...