Na Said Mwishehe,Michuzi TV
RAIS DK.John Magufuli amesema kwamba bila mzee Benjamin Mkapa ambaye ni Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, yeye asingekuwepo hapo alipo leo na kwamba yeye ndio shujaa wake na mtu muhimu katika historia ya maisha yake.
Akizungumza leo mbele ya malefu ya waombolezaji walioshiriki kuaga kitaifa mwili wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Dk.Magufuli amesema "Bila mzee Mkapa nisengekuwa hapa nilipo, mzee Mkapa ni shujaa wangu na mtu muhimu katika historia ya maisha yangu
"Hata nilipopatwa na shida au changamoto mbalimbali mzee Mkapa hakuniacha, hakutaka nianguke alinilea kama mtoto wake , msinishangae ninavyotokwa machozi, hata mzee Kikwete juzi pale nyumbani alishindwa kujizuia alitokwa na machozi.
"Mzee Mkapa alinielea kama mtoto wake, wakati wote alinionesha upendo mkubwa, kuondoka kwake ni pengo kubwa kwangu, kusema kweli nilimzoea sana mzee Mkapa.Hata leo hii ninapowaona mzee Ali Hassan Mwinyi a mzee Jakaya kikwete wakiwa peke yao naumia sana.
"Walikuwa kama mapacha, nimesikitika kuona wamebaki wawili tu , hii inaumiza sana, mtambuka siku za karibuni mmeona hawa viongozi wa tatu walikuwa kwenye uzinduzi wa kitabu cha mzee Mkapa, walikuwa pamoja kwenye uzinduzi wa TASAF Awamu ya tatu, kwenye jiwe la msingi la Ikulu ya Chamwino walikuwa pamoja, kwenye mkutano Mkutano Mkuu CCM walikuwa pamoja, hakika ilikuwa inapandeza ukiwaona, leo hii wamebaki wakiwa wawili , hatutamuona tena,"amesema Rais Magufuli huku akitokwa machozi.
Hata hivyo amesema kwamba alipata nafasi ya kuzungumza naye kwa simu akiwa hospitalini."Nilizungumza naye naye na akaniambia nisiwe na wasiwasi anaendelea vizuri, sikujua kama yale maneno yalikuwa ya kuniaga.Namshukuru Mungu kwa zawadi ya mzee Mkapa, kazi ameikamilisha,"amesema.
Hata hivyo amesema kwa maisha ambayo mzee Mkapa ameyaishi hapa duniani na salamu mbalimbali ambazo zimetolewa zikiwemo za kutoka kwa Baba Mtakatifu Francis ni wazi ameishi maisha yake vizuri hapa duniani na ndivyo vitabu vya dini vinavyofundisha."Tuishi kwa wema duniani na mwisho wa siku tutavishwa taji.
Watanzania tumedhihirisha umoja na mshikamano, nawashukuru viongozi wa dini wa kuendelea kumuombea marehemu. Navishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimamia amani na utulivu, vyombo vya habari, wasanii waliotunga nyimbo mbalimbali kuhusu mzee Mkapa.
"Nawashukuru kwa namna ya pekee wageni wetu kutoka nchi mbalimbali, uwepo na salamu zenu umetupa faraja sana. Napenda kuitumia fursa hii kuipongeza Kamati ya mazishi kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kuifanya katika kipindi hiki cha maombolezo ya mzee wetu.Waendelee kufanya hivyo na siku ya kesho ambayo tutampumzisha mzee wetu kule kijijini kwake Lupaso."
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...