Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU
mkoa wa Njombe,imefanikiwa kuwahoji baadhi ya watia nia wa Ubunge wa
majimbo,Viti maalum na Udiwani waliokuwa wakigombea nafasi ya kupigiwa kura za maoni
katika mchakato uliokamilika hivi karibuni huku wakihusishwa na vitendo vya
rushwa.
Katika taarifa ya kipindi cha mwezi Aprili-Juni
2020, iliyotolewa na mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Njombe Bi,Domina Mukama kwa
waandishi wa habari,amesema wamefanikiwa kuwafuatilia watia nia wote wakiwa
kwenye harakati za kutafuta ridhaa huku baadhi yao wakihojiwa na kuchukuliwa
maelezo yaliyopelekwa katika ngazi nyingine kwa ajili ya maelekezo zaidi.
“Tumeweza kuwafuatilia watia nia wote wa Ubunge wa
majimbo,viti maalum na udiwani wakiwa
kwenye harakati zao za kutafuta ridhaa kutoka kwa wajumbe watakao wapigia
kura,baadhi yao wamehojiwa na hatua stahiki zilichukuliwa dhidi yao”alisema
Domina Mukama
Vile vile amesema TAKUKURU kwa kushirikiana na
vyombo vingine vya usalama wameendelea na zoezi la urejeshaji wa fedha
zilizokuwa zimefanyiwa ubadhiliwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya
ushirika,SACCOS,AMCOS na NJOCOBA.
“kwa kipindi cha mwezi April –Juni 2020 tumefanikiwa
kuokoa kiasi cha Shs.1,001,060,703.99.Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza
wananchi wote wa mkoa wa Njombe waliojitokeza kulipa madni na ninaendelea
kuwaomba wale wote ambao hawajatimiza kulipa madeni yao waendelee kulipa na
kuyamaliza kabisa ili wawe huru.Na kwa wale waliotoroka au kukimbia waelewe tu
kwamba serikali ina mkono mrefu na tutawakamata popote pale walipo”aliongeza
Mukama
Aidha TAKUKURU mkoa wa Njombe imesema kwa kipindi
cha mwezi April hadi Juni wamefanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo katika
sekta ya elimu,afya na maji.
“Katika ya elimu tulikagua ujenzi wa madarasa 4 na
ofisi 4 shule ya sekondari Matola halmashauri ya mji wa Njombe,madarasa 3 shule
ya sekondari Mabatini halmashauri ya mji Njombe,Ujenzi wa madarasa 3 shule ya
sekondari Igima halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe,Ujenzi wa bweni la
wasichana shule ya sekondari Maguvani halmashauri ya mji Makambako,ujenzi wa wa
madarasa shule ya sekondari Makonde katika halmashauri ya wlaya ya Ludewa na
ujenzi wa jengo la udhibiti elimu halmashauri ya wilaya ya Makete”alisema
Mukama
Katika sekta ya afya amesema miongoni mwa majengo
waliyokagua ni pamoja na ujenzi wa zahanati ya Kitole katika halmashauri ya
wilaya ya Njombe,Ujenzi wa zahanati Isindagosi Wanging’ombe.
Amesema katika sekta ya maji walifanya ukaguzi wa
mradi wa maji Matamba-Kinyika katika halmashauri ya wilaya ya Makete,huku
miradi yote iliyokaguliwa imetekelezwa vizuri.
Hata hivyo ametoa kwa wananchi katika kipindi hiki
hiki cha uchaguzi kutokubali kurubuniwa kwa namna yoyote kwa kupewa rushwa ya
fedha au kitu chochote kinacholenga kutoa ushawishi wa kupigiwa kura na
wagombea.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...