WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema suala la ulinzi wa nchi ni la Watanzania wote na siyo la kuwaachia vyombo kama Jeshi la Wananchi, Uhamiaji, Polisi au Magereza.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumapili, Julai 19, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Matogoro, wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara.

“Suala la ulinzi ni letu sote na siyo la Serikali peke yake kupitia wanajeshi au polisi. Kila Mtanzania anawajibika kuilinda nchi hii, kuanzia nyumbani kwako hadi kwa jirani yako. Niwakumbushe kwamba tunapaswa tuendelee kujenga utamaduni wa kutoa taarifa, kila unapoona kuna jambo ambalo una shaka nalo,” amesema. 

Amesema mikoa ya pembezoni ya Kigoma, Kagera, Mtwara, Ruvuma, Katavi, Songwe, Mbeya, Lindi, Mara, Tanga, Kilimanjaro na Arusha ni mikoa ambayo wananchi wake ni lazima wawe wepesi wa kutoa taarifa. “Ni lazima Watanzania tuwe makini, hata kama tuna utaratibu wa kutembeleana, ni lazima tuwe macho.”

Amesema Serikali imeweka mwongozo kwa wageni wanaoingia nchini ambao ni lazima apite kwenye mpaka ulio rasmi na kutoa taarifa zake. “Mgeni huyo atapaswa aeleze amekuja nchini kufanya nini, amekuja na nani na atakaa kwa siku ngapi.”

“Tunapomuona mgeni huko kijijini, ni lazima tujiridhishe kuwa mgeni huyo amepitia kwenye sehemu zote husika. Kama mtu utaona shaka, toa taarifa kwa mtendaji naye atapeleka taarifa hizo ngazi za juu hadi kwa Mkuu wa Wilaya.”

Amesema kila mwananchi atakapojiridhisha kuwa nchini kuna amani, kutakuwa na hali ya utulivu ambayo ni muhimu kwa usalama wa ndani na nje.

Amesema wilaya za Masasi, Nanyumbu na Mtwara Vijijini ni maeneo yanayovutia watu kuingia nchini kwa sababu ya zao la korosho na biashara zilizopo.

 “Hapa Tandahimba kuna mzunguko mkubwa wa fedha. Tandahimba ina idadi kubwa ya wafanyabiashara, hivyo ni rahisi kwa mtu kuja kufanya ujambazi au kuiba mazao yenu. Tunataka muwe macho, lengo letu ni kuhakikisha eneo hili lisiwe moja ya maeneo hatarishi,” amesisitiza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...