Wananchi Kijiji
cha Mwanzugi Igunga wakipata huduma ya Maji kwenye vioski vilivyojengwa kupitia
mradi wa usafirishaji wa maji Ziwa Viktoria kwenda Tabora. 
Tanki la maji
linalohudumia mji wa Igunga.
Wadau wa Sekta
ya maji wakishuhudia maji yalivyofika katika nyumba za wananchi mjini Tabora
Na,
Evaristy Masuha.
Kuna
msemo wa Kikerewe kwamba ‘Alya ebhihile niwe atagata.’ Tafsiri isiyo rasmi ya
Kiswahili ni kwamba alaye vilivyoiva ndiye hupata joto. Msemo wa Kiswahili
unaofanana na huu ni ule usemao, ‘aisifuye mvua imemnyeshea.’ Moja ya kundi
kubwa ambalo linasadifu ukweli wa misemo hii ni wananchi wa mikoa ya Tabora,
Shinyanga, Mwanza na Geita. Hawa wamenena kwa lugha tofauti tofauti. Kubwa
zaidi ni kuipongeza serikali kwa kuwezesha maji ya ziwa Victoria kufika katika
miji yao na hatimaye kuondoa changamoto ya upungufu wa maji katika miji hiyo.
Taarifa
ya Wizara ya Maji kuhusu miji ya Nzega, Tabora, Igunga na Uyui, inaonesha kuwa
Februari mwaka huu 2020 miji yote hiyo pamoja na vijiji 92 vilivyoko maeneo
hayo vimefikiwa na huduma ya maji, wakati
vijiji kumi vikitarajiwa kufikiwa hivi karibuni.
Hili
jambo siyo dogo kwa sababu maeneo hayo yamekuwa na hali ya ukame na upungufu wa
maji ambao umekuwa ukienda sambamba na
ukosefu wa huduma ya majisafi na salama ya kutosheleza kwa saa zote, bila mgao.
Hali hiyo imechangia kuathiri kwa kiasi
kikubwa maendeleo ya wakazi na wananchi wengine. Magonjwa ya kuambukiza hasa
yale yanayotokana na matumizi ya maji yasiyosalama yamekuwa yakitajwa sana katika maeneo haya.
Malalamiko na mrejesho wa wananchi hao umeifikia serikali na kufanyiwa kazi.
Ni
jambo lililowazi kuwa Awamu hii ya tano imesikia kilio cha wananchi katika
maeneo haya na hatimaye kuwafikishia huduma hiyo muhimu ya maji. Mafanikio ya upatikanaji wa huduma ya maji ya
uhakika ni kuashiria safari mpya ya mafanikio katika nyanja zote za Maisha.
Kwenye
mitandao ya kijamii ikiwemo youtube yenye viunganishi https://www.youtube.com/watch?v=3mbOrDftDwg Pamoja na https://www.youtube.com/watch?v=0wG6iVJiIOk Wananchi wa miji hii wamesikika wakipaza
sauti zao kuishukuru serikali kwa kusikia kilio chao.
Mkuu
wa Mkoa wa Tabora (mstaafu) Ndugu Aggrey Mwanri ambaye amekuwa akisikika mara
nyingi kwa mipango ya kuifanya Tabora kuwa kama jiji la Toronto, kwa bara la
Afrika anasema maji yameileta Toronto ya kweli aliyoihubiri kwa muda mrefu.
Anaenda mbali kwa kueleza kwamba changamoto ya magonjwa yanayotokana na
matumizi ya maji machafu ikiwemo homa ya matumbo na magonjwa ya kuhara
imepungua sana mkoani Tabora mara baada ya mradi mpya kufikisha maji katika
maeneo ambayo hayakuwa na huduma. Zaidi,
pamoja na hilo anawaalika wawekezaji kuelekea
mkoani Tabora kwani changamoto kubba za mkoa huo ikiwemo huduma ya maji
Serikali imezitatua.
“Hakuna
mwekezaji anayetamani kwenda kuwekeza katika eneo ambalo lina uhaba wa maji.
Toronto ya kweli sasa imefika. Niwaombe Watanzania wote, wakiwemo wakazi wa
Mkoa wa Tabora walioko ndani na nje ya nchi waje kuwekeza nyumbani”, Mhe. Mwanri anasema.
Bi.
Pili Mweda ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mwanzugi wilayani Igunga anasema
walikuwa na kawaida ya kuchangia matumizi ya maji na mifugo wakati huo
wakitegemea maji kutoka bwawa la Mwanzugi. Naye Edina Philipo Mkazi wa Igunga
anasema iliwahi kutokea wakavamiwa na watu ambao walishindwa kuwatambua wakati
wakienda kuchota maji nyakati za usiku.
“Mimi
mwenyewe niliwahi kukimbizwa usiku nikifuata maji. Bahati nzuri nilikimbia nikapiga
kelele aliyekuwa akinikimbiza akaniacha. Kwa kweli ujio wa maji haya umepunguza
matatizo mengi ya kifamilia huku kwetu”.
Mathias
John, Mkazi wa Ziba Kitongoji cha Igumila wilayani Nzega anasema uhaba wa maji
ulikuwa umeleta utaratibu mpya wa maisha. Badala ya utaratibu wa kawaida wa
maji kuchotwa na akina mama, kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na akina baba kwa
kutumia maguta, mikokoteni au baiskeli.
Akiongelea
mabadiliko baada ya mradi mpya kuanza kazi, Elifuraha Keflasi Mpanda anayeishi
Mtaa wa Mwayunge Wilayani Igunga ambaye anasema maji yamemfanya aione fursa
mpya ya kilimo cha bustani ya Mbogamboga na ufyatuaji wa matofali kwa ajili ya
biashara.
“Nafurahi
sasa nimeiona fursa mpya. Nafyatua matofali, nauza, nalima bustani na kuzalisha
mbogamboga ambazo zinaniongezea kipato”.
Mbali
na wananchi mkoani Tabora uongozi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
wilayani Igunga ukiongozwa na Mkurugenzi
wa Mamlaka hiyo Mhandisi Rafaeli Melumba anasema kabla ya mradi kuna wakati
serikali ilikuwa inalazimika kuingia gharama kubwa kusomba maji kuwapelekea
wananchi kwenye maeneo yao.
“Kwa
mfano mwezi wa kumi mwaka jana tulilazimika kuingia gharama ya kusomba maji
kuwapelekea wananchi kwenye maeneo yao kutokana na ukame uliosababisha kukauka
kwa mabwawa yote likiwemo bwawa la Bulenya ambalo wamekuwa wakilitegemea.” Mhandisi Melumba anasema.
Vilio
vyote hivi vinaonesha jinsi tatizo la maji lilivyokuwa kubwa katika maeneo
hayo. Shida hiyo ilikuwa imezalisha utamaduni mpya wa maisha, ugumu wa maisha
ulikuwa umebadilika kuwa hali halisi ya maisha ya Igunga. Sasa hali
imebadilika. Ujio
wa maji unafungua fursa nyingi za kiuchumi mkoani Tabora na kupunguza gharama
za maisha kwa familia za wananchi.
Mmoja
wa wanufaika wa mradi huo Mzee Lumanila Kija wa Kijiji cha Ziba wilayani Nzega
anasema gharama za maji zimepungua kutoka kati ya shillingi 500 hadi 1000 kwa
ndoo na kwa sasa kuwa shilingi 30 hadi
50 kwa ndoo. Mzee anasemia kama sio umri wake, angekuwa bado ni kijana,
angeweza kufanya makubwa kwa sababu alishindwa kufanya mengi wakati wake
kutokana na sehemu kubwa ya maisha yake
kutumia muda mwingi katika utafutaji wa
maji kwa matumizi mbalimbali ya familia.
Maji
yamefungua fursa mpya za kibiashara. Adamu John wa kijiji cha Ziba anasema ujio
wa maji umemfanya aanze biashara ya kuchuuza
maji ambapo kwa sasa anawapelekea wananchi majumbani mwao hasa wale
ambao hawana nafasi ya kufika kwenye vioski vilivyojengwa na serikali kwa ajili
ya kutoa huduma hiyo kwa wananchi wote. Kazi hiyo imemuwezesha kununua baiskeli
mpya na kuanza ujenzi wa nyumba ya kudumu.
Maji
yameleta fursa ya kilimo cha biashara. Sadda Juma mkazi wa Nzega anasema sasa
anaweza kulima mbogamboga kwa ajili ya chakula cha familia na ziada anayoipata
anafanya biashara.
Agostino
Petro Maridadi, Mkazi wa Mwanzugi Igunga anasema sasa ni mfanyabiashara wa
tofali. Anafyatua, kuchoma na kuuza. Hilo limemsaidia kujikwamua kiuchumi na
kukidhi mahitaji ya familia na kuwasaidia ndugu zake wengine katika shughuli
mbalimbali za kijamii.
Hili
ni jambo kubwa na la faraja kwa wananchi. Ni jambo ambalo Serikeli yoyote
inayojali maslahi ya umma italizingatia. Heri kwa wana-Igunga, Heri kwa
Watanzania. Heri kwa Serikali ya awamu ya Tano. Ndoto ya kumtua mama ndoo
imetimia na kazi inaendelea katika maeneo mengine kuwaletea huduma ya maji
Watanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...