Prof. Museru na Dkt. Magandi
wakiwa wameshika moja kati ya vifaa tiba vilivyokabidhiwa hospitalini
hapa kinachotumika kupima kiwango stahiki cha gesi katika vifaa tiba
vinavyotumia gesi (Portable Gas Flow Analyzer).

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza kabla ya
kukabidhiwa msaada wa vifaa tiba kutoka Taasisi ya Korea Foundation for
International Healthcare (KOFIH), kulia ni Kaimu Naibu Mkurugenzi
Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi, kushoto ni Mwakilishi wa
KOFIH Bi. Kim Jungyoon.
…………………………………………………………………………
Hospitali ya Taifa
Muhimbili-Mloganzila imepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya
TZS. Mil 331,383,000 kutoka Korea Foundation for International
Healthcare (KOFIH) ambao unalenga kuisaidia hospitali kuendelea kutoa
huduma bora na za ubingwa wa juu kwa wagonjwa wanaofika kupatiwa
matibabu hospitalini hapa.
Msaada huo umejumuisha vifaa tiba
vya kufanyia upasuaji masikio, pua na koo vilivyogharimu Dola za
Marekani 41,826 sawa na TZS. Mil. 96,199,800 na vifaa vya ufundi kwa
ajili ya matengenezo ya vifaa tiba vyenye thamani ya dola za marekani
102,254 sawa na TZS. Mil. 235,184,200.
Akipokea msaada huo Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru
ameishukuru taasisi hiyo kwa kuendeleza mahusiano na MNH pamoja na
kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano kwa kuwajengea uwezo
wataalamu kupitia mafunzo mbalimbali na pia katika kuimarisha utoaji
huduma kwa kutumia vifaa tiba vilivyopo hospitalini hapa.
“Changamoto tuliyonayo ni
utengenezaji wa vifaa tiba tulivyonavyo pindi vinapopata hitilafu lakini
kupitia ushirikiano mzuri tulionao na KOFIH umewezesha wataalamu wetu
kupata ujuzi na vifaa kwa ajili ya matengenezo ambayo yamewezesha
hospitali kuendelea kutoa huduma pasipo shida yoyote,” amesema Prof.
Museru.
Mwakilishi wa Taasisi ya Korea
Foundation for International Healthcare, Bi. Kim Jungyoon amesema
wanayofuraha kukabidhi msaada huu ambao utasaidia wataalamu wa upasuaji
masikio,pua na koo pamoja na wataalamu vifaa tiba kufanya kazi zao kwa
ufanisi.
“Tunaishukuru Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa kuendeleza mahusiano haya nasi tunaahidi kuendelea
kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha wataalamu wanapatiwa mafunzo
na vifaa tiba vitakavyowasaidia wakati wa kutimiza majukumu yao ya kila
siku,” amesema Bi. Jungyoon.
Mwishoni mwa mwaka jana KOFIH
ilitoa mafunzo ya mwezi mmoja kwa wataalamu wa vifaa tiba kutoka Dar es
Salaam, Dodoma, Tabora, Lindi, Tanga, Geita, Mwanza, Arusha, Pwani,
Mtwara, Singida, Mbeya, Kilimanjaro, Shinyanga na Katavi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...