Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Young Scientists(YST) imewatangaza wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Ngaza ya jijini Mwanza Glory Kirochi na Martha Machumu kuwa washindi wa tuzo ya wanasayansi chipukizi ambayo hutolewa na taasisi hiyo.
YST imesema wanafunzi hao wameibuka washindi baada ya kubuni mradi wa namna ya kuzalisha chakula cha mifugo katika kipindi cha ukame (hydroponic fodder).
Akizungumza katika utoaji wa Tuzo hizo uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, Mwanzilishi mwenza wa YST, Dk Gozberth Kamugisha amesema washindi hao wamepata kikombe, ngao, medali na fedha Sh.1,350,000.
Mbali ya zawadi hizo pia wamepata ufadhili wa masomo yao ya elimu ya chuo kikuu kwa kulipiwa gharama zote na Taasisi ya Karimjee Jivanjee.
Amesema nafasi ya pili ilichukuliwa na wanafunzi kutoka mkoani Arusha katika Shule ya Kisimili ambao ni Albert Mhagama na Stella Kasalla ambao walipata kikombe, ngao, medali na Sh.900,000.
Pia amesema tuzo ya kumbukumbu ya Hatim Karimjee ilichukuliwa na Rugambwa Sekondari iliyopo mkoani Kagera ambapo wanafunzi Ivony Rio na Dorris Kilonzo waliokuwa na mradi wa kuboresha usalama wa ndani ya gari ambapo wamepata Sh milioni moja, ngao na medali .
Aidha amesema Lameck Obeid na Dennis Ndahaje wa Shule ya Sekondari ya Katubuka iliyopo Kigoma walipata ufadhili wa masomo baada ya kuja na mradi wao waliouita ‘siri kwa nini wanafunzi wanaotoka familia duni wanashindwa kufikia malengo ya elimu’.
“Hii ilitufanya tubadilishe mifumo yetu na kutumia njia za kidigitali kuwafikia wanafunzi na majiji kukagua kazi hizo na kufanya maamuzi kupitia mtandao,” amesema Kamugisha.
Ameongeza kwamba na maonesho hayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuongeza chachu kwa wanafunzi kupenda masomo ya sayansi lakini mwaka huu kutokana na changamoto ya Covid-19 yameshindwa kufanyika zaidi ya kutoa tuzo hizo kwa njia ua mtandao.
Hata hivyo amesema wakiwa wanasherekea kufikisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, wana mengi ya kujivunia kwa kuzifikia shule nyingi zaidi na kuleta mabadiliko makubwa katika nyanja ya sayansi na teknolojia.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee ambao ndio wadhamini wakuu, wa maonesho hayo Yusufu Karimjee amefafanu kwamba mpaka mwaka jana jumla ya wanafunzi 29 waliofanya vizuri katika YST wanafadhiliwa masomo yao ya elimu ya juu.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Nganza iliyopo jijini Mwanza, Glory Kirochi na Martha Machumu wakiwa meshikilia kikombe walicho kabidhiwa baada ya kuibuka washindi wa tuzo ya wanasayansi chipukizi inayotolewa na Taasisi ya Young scientists Tanzania(YST) jana jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...