Na Mohamed Saif
Wananchi
wa Kijiji cha Bulongwe Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya waimeipongeza
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Maji kwa jitihada zake za
kuwaondolea kero ya maji iliyowasumbua kwa kipindi kirefu.
Pongezi
hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti Julai hapo juzi wakati wa ziara ya
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ya kukagua
utekelezaji wa miradi ya Maji Mkoani humo na kuzungumza na wanufaika wa
miradi hiyo.
Akiwa kwenye
mradi wa Masoko Skimu ya Bulongwe Wilayani Rungwe, Mhandisi Sanga
alisema kuwa wakati wa kampeni za Urais Mwaka 2015, Rais Dkt. John Pombe
Magufuli aliahidi kuwa wananchi hao watafikiwa na huduma ya majisafi na
salama na kwamba ziara yake wilayani humo imelenga kukagua utekelezaji
wa ahadi hiyo sambamba na kubaini changamoto zilizopo kwa lengo la
kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
"Rais
Magufuli aliahidi na alituelekeza kuhakikisha wananchi wake wa Rungwe
wanapata huduma ya maji, nipo hapa kukagua utekelezaji wa maelekezo hayo
pamoja na kuona namna ya kuboresha zaidi huduma ya maji kwa wananchi
wasiokuwa na huduma" alisema Mhandisi Sanga.
Aidha,
akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kijiji cha Bulongwe Mwenyekiti wa
Kijiji, Gibons Mwapangala alisema kero ya maji ilikuwa ni ya muda mrefu
lakini kupitia Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kero hiyo imekuwa historia.
“Kiukweli
kwa niaba ya wananchi wa Bulongwe ninampongeza na kumshukuru sana Rais
wetu, kero ya maji ilitusumbua sana, lakini yeye alipita hapa na
alituahidi kwamba tutapata maji na kweli tumeyapata,” alisema
Mwapangala.
Hata hivyo
alibainisha kwamba kuna maeneo machache ambayo bado hayajafikiwa na
huduma na alimuomba Katibu Mkuu Sanga kufikisha huduma kwenye maeneo
hayo.
Kwa upande wake
Mhandisi Sanga aliielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Mbeya (Mbeya UWSA) kukutana haraka na wananchi ambao bado
hawajafikishiwa huduma na alitoa Siku 14 maeneo yote ambayo
hayajafikishiwa yawe yamefikishiwa huduma.
"Nawaelekeza
Mamlaka ya Maji Mbeya pamoja na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Wilaya
ya Rungwe kukutana na wananchi wa Bulongwe siku ya Jumatatu Agosti 10,
2020 na mhakikishe ndani ya Siku 14 kutoka sasa muwe mmewafikishia
maji," alielekeza Mhandisi Sanga.
Aidha,
akiwasilisha taarifa ya mradi, Mhandisi wa Maji, Mamlaka ya Maji Mbeya
(Mbeya UWSA), Raphael Kolong'onyo alisema mradi huo unatekelezwa na
wataalam wa ndani kwa mfumo wa force account na kwamba utekelezaji wake
ulianza Septemba, 2019 na hadi hivi sasa ujenzi wake umefikia asilimia
97.
"Tayari baadhi ya
wananchi wanapata huduma lakini wachache tunaendelea kuwasogezea kwani
tunatarajia kuukamilisha hapo Septemba, 2020 na utakuwa umegharimu jumla
ya shilingi milioni 547," alisema Mhandisi Kolong'onyo.
Kukamilika
kwa mradi huo wa Bulongwe kutanufaisha zaidi ya wananchi 10,000 kutoka
vijiji sita ambavyo ni Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Bujera na
Nsongola.
Mkuu wa Wilaya
ya Rungwe, Chalya Nyangindu akitoa taarifa ya Sekta ya Maji ya Wilaya
ya Rungwe kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha
Bulongwe, Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wakati wa ziara ya kukagua
ujenzi wa miradi wilayani humo.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akiwasikiliza wananchi
wa Bulongwe (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa
maji Bulongwe. Kulia ni Mhandisi wa mradi kutoka Mamlaka ya Majisafi na
Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA), Raphael Kilong’onyo.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akiwasikiliza wananchi
wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa maji Bulongwe.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...