Yassir Simba, Michuzi Tv
Achana na lile pira gwaride liliyopigwa pale katika dimba la Nelson Mandela mjini Sumbawanga rejea tena katika mchezo mkali wa ligi kuu Tanzania bara VPL uliopigwa Oktoba 22,2020 ukiwakutanisha Tanzia Prisons dhidi ya Simba Sports Club ya jijini Dar es Salaam ambapo wapenzi wa kabumbu nchini walishuhudia Mnyama kwa mara ya kwanza katika msimu huu wa ligi 2020/2021 akipoteza mchezo wake wa kwanza.
Mchezo huo uliotawaliwa na matumizi ya nguvu kwa asilimia kubwa kwa upande wa Tanzania Prisons huku vita kali ikiwa kati ya beki kisiki wa timu hiyo Benjamin Asukile dhidi ya Luis Miquissone wa Simba, Mchezo huo ulishuhudia kwa mara ya kwanza Simba ikicheza bila ya wachezaji wake hatari Kagere,Chama pamoja na Mugalu huku ikianza na Charles Ilamfya kama mshambuliaji wa kati ambaye alishindwa kuipenya ngome ngumu ya ulinzi ya timu ya Tanzani Prisons ikiongoza Benjamini Asukile pamoja Michael Ismail ambao walisimama imara katika dakika zote tisini za mchezo.
Mpira wa krosi uliopigwa na beki wa Tanzania Prisons Michael Ismail katika dakika ya arobaini na nane ya mchezo na kazi yake kumaliziwa na mshambuliaji hatari wa timu hiyo Samson Mbangula kwa kichwa kikali kilichomshinda mlinda mlango wa timu ya Simba Aishi Manula na kuipatia Tanzania Prisons bao la kuongoza na la ushindi katika mchezo huo.
Hadi dakika tisini za mchezo zinamalizika zilishuhudia Tanzania Prisons wakitaka katika uwanja wao wa NYUMBANI kwa kulizuia pira biriani la Wekundu wa Msimbazi Simba na kushuhudia Mnyama akipoteza mchezo wake wa kwanza katika ligi kuu ya Tanzania bara VPL.
Rasmi Tanzania Prisons wanajikita katika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi kuu wakijikusanyia alama tisa katika michezo saba huku Mnyama Simba akishuka hadi nafasi ya tatu akiwa na alama kumi na tatu mara baada ya kucheza michezo sita akiwa nyuma kwa alama nane dhidi ya kinara ligi Azam FC mwenye alama ishirini na moja.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...