Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa mtaa wa Mtakuja katika kata ya Chang’ombe jijini Dodoma tarehe 18 Desemba 2020 alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu katika mtaa huo. Kushoto kwa Lukuvi ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge.
*************************************
Na Munir Shemweta, DODOMA.
Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ametangaza eneo lenye
mgogoro wa muda mrefu la Mtakuja katika kata ya Chang’ombe mkoani Dodoma
kuwa la Makazi na kuanza zoezi la urasimishaji litakalookoa takriban
bilioni 8.5 zilizokuwa zitumike kufanyiwa maboresho.
Eneo la Mtakuja awali
lilipangwa kama eneo la ukanda wa kijani na iliyokuwa Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa ajili ya kutunza mazingira na baadaye
kupangwa kwa matumizi ya makuburi na kuvamiwa na hivyo kuingia katika
mgogoro mkubwa na wananchi kufuatia kutangazwa kufanyiwa maboresho na
halmashauri ya jiji la Dodoma.
Lukuvi alitangza
uamuzi huo tarehe 18 Desemba 2020 katika mtaa wa Mtakuja jijini Dodoma
alipozungumza na wananchi wa mtaaa huo akiwa katika ziara yake ya
kushughulikia migogoro ya ardhi nchini.
Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, kufuatia uamuzi wa kulitangaza
eneo hilo kurasimishwa sasa eneo hilo litapimwa na kupangwa upya na
hakuna mwananchi atakayevunjiwa nyumba na kila mtu atapata haki yake.
Kwa mujibu wa Lukuvi,
timu ya wizara kwa kushirikiana na halmashauri ya jiji la Dodoma
itaanza kazi ya urasimishaji wiki ijayo na kukamilika mwishoni mwa mwezi
februari 2021 kwa wananchi kupatiwa hati za umiliki.
“urasimishaji
utakaofanyika utafuta maendelezo ya kila mwenye eneo bila kubomoa
nyumba ya mtu, tunataka kila mwanachi apate haki yake na awe na uhakika
wa makazi yake ya kuishi” alisema Lukuvi.
Aidha, Waziri wa
Ardhi alisema kila mwananchi katika eneo la Mtakuja atalazimika
kugharamia gharama za upimaji mpaka umilikishwaji na zile kodi za
kisheria na kusisitiza kuwa anaamini hakuna mwananchi atakayeshindwa
kulipia.
Lukuvi alibainisha
kuwa, kwa wale wananchi waliopewa maeneo lakini hawakujitokeza wakati wa
uhakiki zoezi la utambuzi litaendelea ili kila mmoja apate haki yake.
Wananchi 867 wamehakikiwa kati ya 1049 na hivyo kufanya wananchi 182
ndiyo pekee wasiohakikiwa.
Kufuatia uamuzi wa
kutangaza eneo la Mtakuja kurasimishwa sasa hati zote za wamiliki wa
ardhi katika eneo hilo zimefutwa. Eneo hilo lilikuwa na jumla ya hati
65 zilizokuwa zimetolewa kwa baadhi ya wananchi wa Mtakuja.
Waziri Lukuvi
alitangaza pia kufanyika uhakiki upya katika maeneo ya wananchi
waliopitiwa na barabara za mzunguko katika eneo la Mtakuja ambapo awali
uhakiki ulifanywa na Wakala wa Barabara TANROADS. Kwa mujibu wa Lukuvi
lengo la kufanya uhakiki upya ni kubaini udanganyifu uliofanywa na
baadhi ya wananchi wasio waaminifu waliokuwa na lengo la kujipatia kiasi
kikubwa cha fedha ya fidia.
Kwa upande wake Mkuu
wa mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge alilitaka jiji la Dodoma
kuhakikisha maeneo yenye maboresho yanafanyika kwa kasi ili kuepuka
madhara yanayoweza kutokea kama ilivyokuwa kwenye eneo la Mtakuja
alilolielezea madhara yake yametokana na uzembe wa kutofanya maboresho
mapema.
Mbunge wa jimbo la
Dodoma Mjini Anthony Mavunde kwa niaba ya wananchi wa eneo hilo
alimpongeza Waziri wa Ardhi William Lukuvi kwa juhudi kubwa alizozifanya
hadi kuutatua mgogoro huo ambao uhakiki wake ulikwama mara mbili mpaka
alipoingilia kati.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...