MKUU wa Mkoa wa Ruvuma
Christina Mndeme amefungua Jukwaa la kuimarisha uhifadhi ushoroba wa Selous
Niassa ambalo limefanyika kwa siku mbili
kwenye ukumbi wa Heritage Cottage mjini Songea.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa Jukwaa hilo Mndeme amewaagiza wadau wa uhifadhi mkoani Ruvuma
kuhakikisha kuwa ushoroba wa wanyamapori wa Selous Niassa unaimarika na kufikia
malengo ya kunufaisha jamii za kizazi cha sasa na kijacho.
“Eneo la ushoroba wa
Selous Niassa limebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali mbalimbali za
mimea,wanyamapori,ndiyo maana Pori la Akiba la Selous limechaguliwa na UNESCO
kuwa urithi wa dunia na kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.’’alisema
Mndeme.
Amesema ushoroba huo
una makundi makubwa ya wanyamapori kama tembo,mbwamwitu,nyati,viboko na simba
na kwamba ushoroba huo ni muhimu kwa hifadhi mbili za Tanzania na Msumbiji
yaani Selous na Niassa.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo
wa Mkoa,sekta ya utalii nchini inaingiza pesa nyingi za kigeni kwa kuwa inaleta
wageni milioni 1.5 kwa mwaka na kwamba utalii pekee unachangia pato la Taifa
kwa asilimia 17 na kutoa ajira kwa watanzania milioni mbili.
Kwa upande wake
Mwakilishi wa Uwanda wa Ruvuma wa Shirika la WWF Diana Shuma amesema jukwaa
hilo la Mkoa ni la pili kufanyika likihusisha ushoroba wa Selous Niassa na
kwamba kikao hicho kinawakutanisha wadau ili kujadili namna ya kuhifadhi
ushoroba huo ambao upo katika hatari ya kutoweka.
Amesema ushoroba huo ni
muhimu kwa Tanzania na Msumbiji kwa kuwa ni mapitio muhimu ya wanyamapori na
unakabiliwa na changamto ya watu kufanya shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo na
ufugaji.
“Lengo la kuanzisha
jukwaa hili ni kuwaleta pamoja wadau
kujadili na kutengeneza mikakati ya kuhifadhi ushoroba huu wa Selous
Niassa ambao una ukubwa wa hekta zaidi ya milioni 1.5.’’alisisitiza Shuma.
Fidel Kimario ni
Mratibu Uhifadhi Wanyamapori na mapito ya wanyama Wizara ya Maliasili na Utalii
amesema serikali imeandaa kanuni za kusimamia mapito ya wanyamapori ili
kukabiliana na hatari ya kutoweka mapito ya wanyamapori.
Enock Msocha ni Kaimu
Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Kanda ya Kusini Mashariki wa TAWA inayohusisha
mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma,amesema wameongeza mbinu mbalimbali za
kulilinda pori la Selous ikiwemo kuongeza doria katika maeneo yote wakati wote.
Hata hivyo amesema
wanashirikiana na wananchi katika maeneo jirani ya hifadhi kufanya ulinzi na
kufuatilia wanyama kwa karibu endapo wamevuka katika maeneo ya wananchi ili
wananchi na wanyama waweze kuwa salama.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...