MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amekabidhi msaada wa taulo za kike 2,502 zilizotolewa na Shirika la Social Action Trust Fund(SATF) kwa wanafunzi wa shule saba za msingi wilayani Nyasa.

Mndeme amemkabidhi taulo hizo na nguo za ndani 834 Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isebala Chilumba katika hafla fupi iliyofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.

Mndeme amezitaja shule ambazo zitakabidhiwa msaada huo kuwa ni  zenye wanafunzi wa darasa la nne hadi la sita  kutoka shule saba za msingi ambazo ni shule ya msingi, Kilosa, Likwilu, Muongozo,Ukuli,Kuhamba,Liparamba na Lumeme.

“Natoa wito kwa Halmashauri ya Nyasa,kuhakikisha inashirikiana na Shirika la SATF,kabla ya matumizi ya vifaa wanafunzi wapewe mafunzo kupitia klabu zao za afya.’’alisisitiza Mndeme.

Amesema  kutolewa kwa vifaa hivyo ni  juhudi za serikali za kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi ya kumhakikishia mtoto wa kike anapata elimu kwa kuhudhuria masomo na anadumu shuleni na kuhitimu masomo yake bila vikwazo.

Naye Afisa Miradi wa SATF Makao makuu Edgar Kihwelo amesema shirika hilo linafanya kazi na  Asasi za kiraia 19 katika mikoa 16 na wilaya 32 za Tanzania Bara.

Amesema tangu kuanzishwa kwa Shirika hilo  watoto wanaishi katika mazingira magumu 193,000 wamesaidiwa na kuwawezesha kupata elimu na kaya zipatazo 900 zimejengewa uwezo kiuchumi.

Kulingana na Kihwelo,katika wilaya ya Nyasa kwenye mradi ulianzishwa mwaka 2019,Shirika limeweza kusaidia watoto wa shule za msingi 103 na watoto wa shule za sekondari  sekondari 80.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo ,Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba amelishukuru Shirika la SATF kwa msaada huo ambao amesema utasaidia kumkomboa mtoto wa kike kielimu na kufikia ndoto zao.

Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma Imanuel Kisongo amelipongeza Shirika la SATF kwa kuunga mkono jitihada za serikali za kumkomboa mtoto  wa kike katika Mkoa wa Ruvuma.

Amesema taulo za kike zitamhakikisha mtoto wa kike anahudhuria masomo hata  katika siku zake za hedhi bila kuathiri masomo yao na kutimiza malengo yao kimaisha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...