KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo
Gerald Kusaya ameuagiza uongozi wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA)
kutatua changamoto za upatikanaji wa pembejeo, mbegu bora na mikopo kwa
wanachama wake husasan walioko vijijini kwa kushirikiana na wizara.
Akizungumza kwenye ufunguzi
wa mkutano mkuu wa MVIWATA Mkoa wa Dodoma leo (08.12.2020) Kusaya amesema hafurahishwi
kusikia malalamiko ya wakulima wadogo kukosa mbolea na mbegu bora au kusikia
wakiuziwa kwa bei ghali wakati umoja wao upo.
“MVIWATA tumieni umoja wenu
kuagiza mbolea kwa mfumo wa pamoja kupitia Wakala wa mbolea (TFRA) ambapo
mtanunua kwa bei nafuu na kusambaza kwa wana chama wenu vijijini. Wizara ipo na
itasimamia kwa karibu ili kuleta unafuu kwa wakulima “ alisema Kusaya
Kusaya aliongeza kusema mtandao huo una jukumu
pia la kutafuta mbegu bora za gharama nafuu za mazao ya mahindi ,alizeti
,mpunga na mengine kwa kuwasilisha mahitaji yao kwenye Wakala wa Mbegu wa Serikali
(ASA).
Aidha wakulima hao katika
risala iliyosomwa na mwenyekiti wa
mtandao huo mkoa wa Dodoma Said Matonya waliiomba serikali kupitia wizara ya
kilimo kusaidia upatikanaji wa mbegu za mazao ya chakula na biashara mapema
kabla ya msimu kuisha na mbegu hizo ziuzwe kwa gharama nafuu.
Matonya alitaja mbegu za
mahindi mfuko wa kilo mbili zinauzwa vijijini kwa gharama ya kati ya Shilingi
10,000 hadi 12,000 hatua ambayo inakwamisha wakulima wadogo kununua hivyo
kujikuta wakipanda mbegu za asili na zisizo na ubora.
“Wakulima tunakabiliwa na
ukosefu wa pembejeo, mbegu bora, mafunzo na mikopo kutokana na kuwa za gharama
kubwa, hivyo serikali itusaidie tupate huduma hizi kwa gharama nafuu” alisema
Matonya .
Akijibu hoja hiyo Kusaya
alisema serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli inawathamini wakulima ndio maana hatua
mbalimbali ikiwemo Wakala wa Mbegu (ASA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea
wameelekezwa kufikisha huduma zao vijijini kwa bei elekezi ya serikali.
“Uwepo wangu hapa leo ni
uthibitisho kuwa serikali inawathamini na kuwajali wakulima wadogo nchini.
Naagiza tena Wakala wa Mbegu nchini (ASA) ahakikishe mbegu bora za mahindi
zinafika Dodoma na mikoa mingine yote na kuuzwa si zaidi ya Shilingi 6,000 kwa
mfuko wa kilo mbili” aliagiza Kusaya.
Katika hatua nyingine Kusaya
ametoa wito kwa MVIWATA kutumia uwepo wa vyuo 14 vya mafunzo ya kilimo vya
serikali (MATI) na vituo 4 vya mafunzo ya wakulima nchini kupeleka wakulima na wanafunzi (vijana) kujifunza mbinu za
kisasa ili wafanye kilimo biashara na cha kisayansi.
Alitaji kituo cha wakulima
wadogo Bihawana kilichopo Dodoma kama sehemu muhimu ambapo MVIWATA wanaweza
kutumia kufundisha wanachama wake namna ya kuongeza tija na ujuzi wa kuendesha
kilimo biashara.
Kusaya aliwashauri na
kuwasisitiza wakulima kupitia MVIWATA kutumia uwepo wa Mfuko wa Pembejeo (AGITF)
unaosimamiwa na Wizara ya Kilimo kwani utawezesha kupata zana bora za kilimo
kama trekta, powertiller, na pembejeo kwa riba nafuu.
“ Mfuko wa pembejeo ni maalum
kwa ajili ya kukopesha wakulima na riba zake ni nafuu kwani kikundi hukopeshwa
kwa riba ya asilimia 6 na mkulima binafsi hukopeshwa kwa asilimia 7 na kufanya
marejesho kwa muda wa miezi 72” alisisitiza Kusaya.
Mkutano huo wa mwaka wa
wanachama wa Mtandao wa Wakulima Tanzania (MVIWATA) mkoa wa Dodoma umehudhuriwa
na wakulima 100 kati ya 800 kutoka wilaya za Dodoma Mjini, Chamwino, Kongwa, Mpwapwa
,Bahi na Kondoa ambapo pia utafanya uchaguzi mkuu .
Mkutano huo unafanyika ukiwa
na kauli mbiu isemayo “MVIWATA Sauti ya Mkulima, Mtetezi wa Mkulima ni Mkulima
Mwenyewe”.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...