Na Muhidin Amri,Mbinga.
KATIBU
tawala wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Mhandisi Gilbert
Simya,amewataka wataalamu wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kutumia
elimu yao,kutafuta na kubuni kubuni vyanzo vipya vya mapato
vitakavyoisaidia halmashauri hiyo kutekeleza mipango yake ya maendeleo
badala ya kusubiri ruzuku kutoka serikali kuu.
Mhandisi Simya
amesema hayo mwishoni mwa wiki mara baada ya kumalizika kwa zoezi la
kuwaapisha madiwani wapya wa halmashauri hiyo lililokwenda sambamba na
uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti.
Alisema, uwepo wa
vyanzo vingi vya mapato kimsingi vitasaidia sana kuongeza makusanyo na
hivyo kukuza mapato yake ya ndani, ambapo halmashauri itaweza
kujitegemea na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kuimarika kwa
huduma za kijamii.
Kwa mujibu wake,kuna baadhi ya miradi ya
maendeleo inayoanzishwa lakini kutokana na ukosefu wa fedha inashindwa
kukamilika kwa wakati,kwa kuwa inasubiri fedha kutoka serikali kuu,
lakini iwapo halmashauri itakuwa na mapato ya kutosha miradi hiyo
itakamilika na kuleta tija kwa wananchi.
Alisema, serikali kuu
ina wajibu wa kuisimamia halmashauri katika suala zima la kukusanya
mapato yake ya ndani na wao kama viongozi watahakikisha wanakuwa wakali
na hata kuwachukulia hatua watumishi watakao shindwa kukusanya na
kusimamia kwa namna yoyote mapato yanayopatikana.
Pia Simya
ameagiza viongozi wa halmshauri hiyo kuwachukulia hatua za kinidhamu
watumishi watakaobainika kukusanya mapato ya halmashauri na kuyafanyia
matumizi bila kupitia benki kwani ni kinyume na maelekezo ya serikali ya
awamu ya tano.
Aidha, amewataka watumishi na madiwani wa
halmashauri kuhakikisha wanashirikiana katika majukumu yao ya kila siku
ili kutekeleza na kutimiza malengo ya halmashauri hiyo pamoja na
maelekezo yote yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Simya
alisema, ili kufikiwa malengo watumishi wa halmashauri kwa
kushirikiana na madiwani wanapaswa kuwa wabunifu wa vyanzo vipya vya
mapato badala ya kubweteka kutokana na mafanikio waliyopata katika mwaka
wa fedha 2019/2020.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Juma
Mnwele alisema, mwaka uliopita walikusanya bilioni 2.9 sawa na asilimia
94 na mwaka huu hadi kufikia mwezi Novemba tayari wamekusanya shilingi
bilioni 1.6 sawa na asilimia 100 ambapo muelekeo wa makusanyo ya
mapato ni mazuri na wana uhakika yatakuwa makubwa zaidi ya mwaka jana.
Alisema,
watumishi wana hali kubwa ya kufanya kazi ikiwemo jukumu la
kukusanya mapato ya ndani ambayo ndiyo uti wa mgongo wa halmashauri
sambamba na kudhibiti matumizi ya fedha zinazokusanywa.
Mnwele
alisema, kama mkurugenzi wa halmashauri ana matumaini makubwa na
madiwani wapya, na amewakumbusha madiwani hao kuhakikisha wanazingatia
viapo vyao vya maadili na kuepuka kutoa matamko ambayo yanaweza
kuirudisha nyuma halmashauri yao.
Alisema, wao kama watendaji wa
shughuli za kila siku watakuwa daraja zuri kati ya madiwani na wananchi
na kuwaomba kuwapa ushirikiano mkubwa watumishi waliopo ili waweze
kutimiza wajibu wao kwa maslahi ya halmashauri,wilaya,mkoa na taifa.
Kwa
upande wake mwenyekiti mpya wa halmashauri hiyo Desdelius Haule
alisema,kipaumbele chake kikubwa ni kuhakikisha anashirikiana na
madiwani wenzake kwa kila jambo ili kuharakisha maendeleo na uchumi wa
Mbinga.
Alisema, madiwani wako tayari kutoa ushirikiano mkubwa
kwa watumishi wa halmashauri hiyo ili kwa pamoja waweze kutekeleza
majukumu,wajibu wao na kuwahudumia wananchi ambao wana hamu kubwa ya
kupata maendeleo hasa kufuatia serikali kuhamishia makao makuu ya
halmashauri eneo la Kihamili kutoka Mbinga mjini.
Alisema, suala
la ushirikiano kati ya madiwani,watumishi na wadau wengine ni jambo la
maana kubwa kwani bila ya ushirikiano hakuna jambo lolote linaloweza
kufanyika katika suala zima la kuleta maendeleo.
Msaidizi
wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani
Ruvuma Analis Komba kulia,akimsaidia kuvaa joho Mwenyekiti mpya wa
Halmashauri hiyo Desdeliu Haule kushoto kabla ya kuanza kwa kikao cha
baraza jipya la madiwani lililofanyika katika Ukumbi wa mikutano shule
ya sekondari Kigonsera wilayani humo, anayeshuhudia katikati makamu
mwenyekiti Bahati Kumbele.Picha na Muhidin Amri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...