Na Shamimu Nyaki – WHUSM
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa
ameiagiza Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kuongeza ubunifu katika
kutoa huduma na kujiendesha kibiashara ili iendane na soko la ushindani.
Waziri
Bashungwa amesema hayo Desemba 14, 2020 alipotembelea Kampuni hiyo
Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kwamba magazeti yanayochapishwa na
kampuni hiyo ni kioo katika kuelimisha umma kwa kuzingatia uzalendo,
hivyo ni nyema yakaongeza kasi zaidi.
“Nawapongeza mnafanya kazi
nzuri, lakini nasisitiza kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kuandaa
na kuchakata habari zenye usahihi na ukweli zitakazosaidia jamii,
tumieni lugha fasaha ya Kiswahili kwa yale magazeti ya Kiswahili, na
endeleeni kuongeza ubunifu kama ambavyo mmeanza kufundisha kupitia
magazeti lugha yetu ya Kiswahili”,alisema Mhe.Bashungwa.
Mhe
Bashungwa ameongeza kuwa atashirikiana na TAMISEMI kuona namna ya
kutumia Kampuni hiyo katika kuchapisha madaftari ya wanafunzi kwakua
Kampuni hiyo ina uwezo wa kufanya hivyo, huku akiongeza kuwa taasisi
za serikali zinatakiwa kutumia Kampuni hiyo katika kuchapisha maandiko,
majarida, vipeperushi na machapisho mbalimbali.
Naye Naibu Waziri wa
Wizara hiyo Mhe. Abdalaah Ulega ameitaka kampuni hiyo kuona namna ya
kuwekeza katika dijitali hasa katika kuweka maudhui ya michezo na Sanaa
ambayo yana watazamaji na wasomaji wengi lakini pia itasaidia kuongeza
mapato.
“Hongereni kwa kazi nzuri, magazeti yanayozaliswa hapa ni
makongwe katika kuhabarisha umma na yanahitaji kufanyiwa mabadiliko ili
yaendane na uhitaji wa wateja”,alisema Mhe.Ulega.
Kwa upande wake
Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi
amesema kuwa Kampuni hiyo imeendelea kufanyiwa maboresho ambapo
watumishi wenye sifa tayari wameingizwa katika mfumo wa mshahara wa
serikali.
Naye Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni hiyo Bibi. Tuma
Abdallah amesema miongoni mwa mafanikio ambayo kampuni imepata ni
kuanzisha Jukwaa la Biashara ambalo linatoa fursa kwa wafanyabiashara
kutangaza biashara zao, huku akieleza kuwa Kampuni hiyo imedumu sokoni
kwa takribani miaka 90 ambayo imepitia vipindi tofauti vya mabadiliko.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...