WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa daraja la Tanzanite wa daraja jipya la Tanzanite (Salander) jijini Dar es Salaam na kwamba ameridhishwa na kasi ya mradi huo.

 

Amekagua ujenzi wa mradi huo leo (Jumanne, Desemba 22, 2020). Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 1.03 na upana mita 20.5 litagharimu  sh. bilioni 243.75 na linatarajiwa kukamilika Oktoba 14, 2021.

 

“Nimekagua mradi na ujenzi wake unaendelea vizuri, sina mashaka na viwango na naamini utakamilika kwa wakati. Watanzania wanasubiri kwa hamu waanze kupita katika daraja hili.”

 

Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ushiriki wa Watanzania katika ujenzi wa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini kwa kuwa inachangia katika kuongeza wataalamu.

 

Ujenzi wa daraja hilo una lengo la kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi ambayo inatumiwa  na magari mengi yanayoingia na kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam.

 

Mkandarasi anayejenga mradi huo ni kampuni ya GS Engineering Corporation kutoka Korea Kusini na hadi Novemba 30, 2020 utekelezaji wake ulikuwa umefikia asilimia 60.8.

 

Awali, Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Christianus Ako alisema hesabu ya mwaka 2017 ilionesha kuwa kiasi cha magari yanayopita kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi kwa siku kuwa ni wastani wa magari 42,000.

 

Alisema hadi sasa mradi umeajiri jumla ya wafanyakazi 590, kati yao asilimia 92 ni Watanzania na asilimia nane tu ni wataalamu kutoka nje ya nchi.

 

Mhandisi Ako alisema mradi huo pia unaendelea kutoa mafunzo kwa wahandisi 24 wa Kitanzania kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (5), wahandisi wahitimu (12) na wanafunzi wa uhandisi kutoka vyuo vikuu (7). “Mafunzo haya yatawajengea uwezo na ujuzi utakaosaidia Taifa hapo baadae.”

 

Kazi za ujenzi wa Daraja la Tanzanite unaohusisha daraja lenye urefu wa KM 1.03 pamoja na barabara za maingilio zenye urefu wa KM 5.02 zikiendelea jijini Dar es Salaam.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...