Charles James, Michuzi TV

NIPO na nyinyi! Ni kauli ambayo ameitoa Mbunge wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi alipofika kujionea changamoto inayowakabili wananchi wake wa Kijiji cha Kidete Kata ya Mngeta ambao hawana kivuko kinachowawezesha kuvuka Mto Mngeta.

Kunambi amefika katika kijiji hiko ikiwa ni muendelezo wake wa ziara ya kutembelea Jimbo lake kwa ajili ya kuwashukuru kwa kumchagua kwa kura nyingi Rais Dk John Magufuli, yeye kuwa Mbunge na madiwani wanaotokana na CCM lakini pia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake kwenye kila kata ambapo jumla ya kata kwenye jimbo hilo ni 16.

Akiwa kijijini hapo Kunambi amejionea changamoto wanayokabiliana nayo wananchi wa eneo hilo katika kuvuka Mto huo wenye Mamba wengi kwa kutumia Mtumbwi mdogo ambao kwa hakika unahatarisha maisha ya wananchi hao.

Akizungumza na wananchi hao baada ya kuvuka Mto huo kwa kutumia Mtumbwi huo kama wananchi wake, Kunambi amewaomba wananchi hao kumpa miezi mitatu hadi ifikapo Mei Mwaka huu ujenzi wa daraja kubwa la kudumu utaanza na kwa sasa anapambana kuhakikisha kinajengwa kivuko cha muda mfupi.

" Ninafahamu changamoto hii inawatesa wanafunzi wetu na hata nyinyi wananchi katika ufanyaji wa shughuli zenu za kilimo, niwaombe mnipe miezi mitatu ya kuanza ujenzi wa daraja kubwa lakini kwa kipindi hiki kifupi hiki nimemwambia Meneja wa Tanroad Wilaya anipe gharama zinazohitajika ili nitafute tujenge daraja la muda hapa, niwahakikishie hadi kufikia Mei tutakua tumeanza ujenzi wa daraja kubwa ili kuondoa kero hii.

Sipo tayari kuona wananchi wangu wa Mngeta mliotuchagua sisi na Rais Dk John Magufuli muendelee kuteseka na kupata changamoto hii ya kuliwa na Mamba, niwahakikishie tutaanza ujenzi wa daraja la muda mfupi wakati huu ambao tunasubiri daraja la kudumu," Amesema Mbunge Kunambi.

Kwa upande wao wananchi wa kata hiyo wamemshukuru Mbunge huyo kwa kitendo chake cha kufika na kujionea changamoto wanayokumbana nayo huku wakimuomba kutimiza ahadi yake hiyo ndani ya muda mfupi ili waweze kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

" Hatujutii kumchagua Kunambi ameonesha jinsi gani yeye ni Mtoto wa Mlimba, kufika kwake na kujionea kero hii ni hatua ya kwanza lakini tayari ametuahidi kujenga kivuko cha muda mfupi huku akisema ndani ya miezi mitatu daraja la kudumu litajengwa, tunamshukuru sana," Amesema Joseph Mathias ambaye ni mkazi wa Kijiji hiko.

Mbunge wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi (wa pili kushoto) akiwa kwenye mtumbwi kuvuka upande wa pili katika kijiji cha Kidete Kata ya Mngeta baada ya kufika kujionea adha wanayokutana nayo wananchi wa maeneo hayo kuvuka katika Mto huo wenye Mamba.
Mwandishi wa Blog ya Michuzi, Charles James (mwenye kofia nyeusi) akiwa kwenye mtumbwi tayari kuvuka Mto Mngeta wenye Mamba.
 Mwandishi wa ITV, Hilda Mushi akiripoti hali ilivyo katika Mto Mngeta Kata ya Mngeta katika Jimbo la Mlimba ambapo wananchi wanapata changamoto ya kivuko.

Mbunge wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi akizungumza na Wananchi wa Kata ya Mngeta ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kwenye kata 16 zilizopo kwenye jimbo lake.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...