Mwamvua Mwinyi,Pwani


WAKALA wa Usambazaji Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imemhakikishia Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Mkoa wa Pwani Michael Mwakamo kuwa adha ya maji katika baadhi ya maeneo Mlandizi na kata ya Kawawa, inakwenda kupatiwa ufumbuzi .

Endapo kutapatikana maji safi na salama ya uhakika katika maeneo hayo ,basi wananchi wataondokana na kero ya kutumia maji ya chumvi .

Mategemeo hayo yametolewa na Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja, aliyeambatana na Mwakamo kutembelea chanzo cha maji cha Mlandizi, iliyolenga kuzungumzia kero hiyo kwa wakazi wa Mlandizi na vitongoji vyake.

Kauli ya Luhemeja imefuatia taarifa ya Mwakamo aliyemwelezea Mtendaji huyo kuwepo kwa kero hiyo,katika baadhi ya maeneo yakiwemo ya Mlandizi, Kibwende, Kisabi na maeneo ya Mtego wa Simba Kata ya Kawawa ambapo baadhi yao wanatumia maji ya chumvi kutoka chanzo cha Ngeta.

Alieleza, DAWASA imeshaanza mchakato wa kufikisha huduma kwenye maeneo yenye changamoto, huku akitaja eneo la Kibwende na maeneo yake yanayokwenda kupata huduma kupitia mradi unaoelekea Mbwawa, Jimbo la Kibaha Mji.

"Nikupongeze Mbunge kwa kuonesha kuguswa na changamoto za wapigakura wako, nikuhakikishie kuwa tumejipanga kupambana na changamoto maeneo yote kuanzia Kibwende, Kidai na mengine, mpaka mwishoni mwa mwaka huu nataraji kazi itakamilika," alisema Luhemeja.

Awali Mwakamo alieleza,wakazi wa Kidai wanaoishi jirani na jengo la Halmashauri wanatumia maji ya chumvi yanayotokea  Ngeta, wakati ni kipande kifupi kutokea yalipoishia maji ya DAWASA .

"Kutokea hapo kwenda vitongoji vya jirani tayari kuna mfumo wa maji yanayotokea Ngeta ambayo yana chumvi ambapo tayari kuna mtandao wa mabomba, nikuombe kama ikiwezekana tuunganishe ya DAWASA ili kuwaondolea changamoto hiyo wapiga kura wetu," alisema Mwakamo.

Kwa upande wao John Pili Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlandizi, Euphrasia Kadala Diwani Kata ya Mlandizi na Abdallah Kido Kata ya Janga walipongeza juhudi za Mbunge huyo, huku wakimtaka Mhandisi Luhemeja awasaidie waondokane na kero hiyo.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...